Mkoa wa Singida umejipanga kuongeza
eneo la uzalishaji wa Alizeti kutoka ekari 631,931 mpaka kufikia ekari Milioni
moja (1,000,000) kwa kutumia wakulima wadogo wakati, wakubwa na vikundi ili
kuongeza uzalishaji wa Mafuta ya alizeti.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa
Mkoa huo Peter Serukamba wakati akihutubia katika mkutano wa ALAT uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Ikungi na kuhusisha wenyeviti wa
Halmashauri Sita, Madiwani wawili kwa kila Halmashauri na Wakurugenzi.
Amesema zao la Alizeti ndio
kitambulisho cha Mkoa huo hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha eneo la
kilimo linaongezeka ambapo RC amebainisha kwamba ushirikiano wa viongozi wa
vijiji na kata pamoja na Maafisa kilimo kuhakikisha wanahamasha wakulima
kuongeza maeneo na vijana kuwekeza katika Kilimo.
Aidha amefafanua kwamba ukuaji kwa
kasi jiji la Dodoma kunatoa fursa kwa Mkoa wa Singida kuzalisha mazao ya
chakula na mafuta kwa kasi huku akibainisha kwamba ufunguliwaji wa barabara za
Singida Mbeya, Singida, Arusha, Singida, Tanga litaongeza soko na ukuaji mkubwa
wa Mkoa huo.
RC Serukamba amefafanua kwamba mpaka
kufikia msimu wa kilimo wa mwaka kesho Singida kutakuwa na wakulima wa aina
Tatu ambao ni wakulima wadogo, wa Kati na wakubwa watakaolima zao la alizeti
ili kukidhi haja ya soko ambalo mpaka sasa bado halijatengemaa.
Hata hivyo amempongeza Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Ikungi Justuce Kijazi kwa kutenga eneo lenye ukubwa wa ekari
elfu 50 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kilimo cha pamoja unaotekelezwa na
Wizara ya Klimo kwa vijana "build better Tomorow" ambapo RC Serukamba
amesema taratibu za kufanya uchambuzi wa kina utaanza ili kujenga Miundombinu
ya Umwagiliaji.
Akimalizia hotuba yake amewaagiza
Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha wanatumia fedha walizopewa kwa
manufaha kabla ya tarehe 30 Juni na kuhakikisha
hakuna fedha inayobaki.
0 Comments