Kocha Mkuu
mpya wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, amekishuhudia kikosi chake kikiibuka
na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Singida United katika Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam jana.
Katika
ushindi huo uliochangiwa na Mganda Emmanuel Okwi aliyetokea benchi na kutupia
mawili katika kipindi cha pili, Simba ilicheza kwa kujiamini zaidi ya wageni
hao.
Lechantre,
ambaye alitangazwa rasmi jana kuwa Kocha Mkuu wa Simba, ni wa kiwango cha juu,
na haijawahi kutokea kwa klabu za hapa nchini kunasa kocha wa kiwango hicho
katika kipindi cha hivi karibuni, imefahamika.
Lechantre
ambaye aliwasili nchini juzi usiku na kuanza mazungumzo na viongozi wa klabu
hiyo ambayo jana mchana yalifikia tamati baada ya kukubaliana, sasa anazima
tetesi za majina kibao ya makocha waliokuwa wakihusishwa kupewa mikoba ya
Mcameroon Joseph Omog.
Moja ya sifa
kubwa ya kocha huyo katika kipindi cha hivi karibuni ni pamoja na kuinoa timu
ya Taifa ya Congo mwaka 2016, ambayo imekata tiketi ya kushiriki fainali zijazo
za Kombe la Dunia zitakazofanyika Urusi baadaye mwaka huu, na sasa amepewa
mikoba ya kuiongoza Simba baada ya viongozi wa klabu hiyo kuamua kuachana na
Mbrazil Fabio Lopez, aliyeko nchini tangu Jumanne.
Mkuu wa
Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, jana alisema Lechantre
atasaidiwa na Mrundi Masoud Djuma, ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo baada ya
kuondoka kwa Omog.
Manara
alisema Lechantre amefuatana na kocha wa viungo, Mohammed Aymen, raia wa
Morocco na baada ya kufikia makubaliano, wanatarajia kukamilisha taratibu za
kupata kibali na hatimaye Mfaransa huyo aweze kuanza kazi yake mapema.
Sifa
nyingine ya Lechantre, ni kwamba analifahamu vema soka la Afrika, kwani aliwahi
kuiongoza Cameroon kuchukua ubingwa wa Afrika mwaka 2000 huku klabu alizowahi
kuzifundisha ni pamoja na Al Ittihad ya Libya, Al Arabi (Qatar), CS Sfaxien na
Club Africaine zote za Tunisia.
Mbali na
kuiongoza Simba kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo linashikiliwa na
Yanga, Mfaransa huyo atatakiwa kuhakikisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ hao
wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa,
wanafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika
yatakayoanza mapema mwezi ujao.
0 Comments