SIMBA SC
imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mwenge SC ya Pemba katika mchezo
wake wa kwanza wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi jioni ya leo Uwanja wa Amaan,
Zanzibar.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Rashid Farahani aliyesaidiwa na Ali Ramadhani
na Suleiman Karim, mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza.
Iliwachukua
dakika mbili tu Simba kupata bao la kuongoza kupitia kwa beki aliyechezeshwa
kwenye nafasi yake ya zamani, kiungo Jamal Mwambeleko aliyemalizia kwa kichwa
krosi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Mwenge
wakasawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wao, Humud
Abdulrahman Ali aliyefumua shuti baada ya pasi ya Seif Pima Ame.
Mshambuliaji
John Bocco aliingia kipindi cha pili, lakini akashindwa kufunga Simba ikitoa
sare ya 1-1 na Mwenge
Pamoja na
timu zote kufanya mabadiliko kipindi cha pili, lakini kupatikana kwa mabao
mengine ilishindikana.
Katika
mchezo uliotangulia leo wa Kundi B, Singida United imeibuka na ushindi wa mabao
3-2 dhidi ya Zimamoto hapo hapo Amaan. Mabao ya Singida yamefungwa na Deus
Kaseke dakika ya saba, Dany Usengimana dakika ya 21 na Kigi Makasi dakika ya
81, wakati ya Zimamoto yamefungwa na Ibrahim Hamad Ahmada ‘Hilika’ katika daika
ya 39 na 84.
Mechi
nyingine ya Kundi B kati ya Yanga SC na Mlandege itafuatia Saa 2:15 usiku
Uwanja wa Amaan pia.
Kikosi cha
Mwenge SC kilikuwa; Mudathir Khamis Mohammed, Omar Khatib Hamad, William
Venence Michael, Yussuf Said Bwanga, Broklyn Bruno Costa, Hassan Ibrahim,
Humoud Abrahman Ali, Mustanji Mussa Mustanji, Seif Pima Ame/Feisal Khamis Juma
dk92, Ali Hamad Said/Juma Omar dk52 na Kambu Zubeir Zinyori.
Simba SC;
Emanuel Mseja, Paul Bukaba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Yusuph Mlipili,
Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Ally Shomari/Kelvin Faru dk60, Said Hamisi, Juma
Luizio/John Bocco dk46, Moses Kitandu/Nicholas Gyan dk46 na Jamal
Mwambeleko/Shiza Kichuya dk46.
0 Comments