Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ametoka Hospitali ya Nairobi nchini
Kenya leo Jumamosi asubuhi kwenda nchini Ubeljiji kwa matibabu zaidi ya
kuurejesha mwili wake katika hali yake ya kawaida.
Lissu ambaye
pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanzania (TLS) ataondoka saa 2.30 asubuhi
ya leo Jumamosi na Ndege ya Shirika la Kenya akiambatana na mke wake, Alicia.
Lissu
ametoka hospitalini hapo ikiwa baada ya matibabu aliyoyapata tangu Septemba 7
mwaka jana baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana
kwenye makazi yake Dodoma.
Mwanasiasa
huyo amesindikizwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na watoto wake
pacha, Augustino na Edward, ndugu zake, viongozi na wanachama wa Chadema.
"Nawashukuru
sana madaktari wa hapa Nairobi na wale wa Dodoma wakiongozwa na Katibu Mkuu (wa
wizara ya afya Profesa Mpoki Ulisubisya waliookoa maisha yangu," amesema
Lissu kabla ya kupandishwa gari la wagonjwa
"Nakwenda
Ubelgiji kwa matibabu, nikirudi mapambano yanaendelea, nawashukuruni nyote
mlioniombea, nawashukuru Wakenya na serikali yao ambao kwa miezi minne nikiwa
hapa walinipa ulinzi wakati wote."
Akizungumza
kwa msisitizo mbele ya wabunge na wanachama wa Chadema waliokuwapo amesema
"Chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya."
Kuhusu
gharama, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema gharama za safari
na matibabu zimegharamikiwa na Chadema na TLS.
Baadhi ya
waliokuwapo hospitalini kumsindikiza Lissu uwanja wa ndege ni kaka yake Alute
Mghwai, mdogo wake, Vinceti Mghwai na ndugu wengine.
Pia, Dk
Mashinji, Naibu Makatibu Wakuu, John Mnyika (Bara), Salum Mwalimu (Zanzibar).
Wengine
walikuwapo ni wabuge wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba) na Godbless Lema(Arusha
Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Rose Kamili (Viti Maalum), Anna Gideria
(Viti Maalum).
Kwa niaba ya
familia, Alute amesema "Tunamwomba Mungu ajalie huko anakokwenda akapate
matibabu, kwani alivyokuja hapa sivyo anavyoondoka na tunawashukuru wananchi wa
Tanzania na Kenya kwa ushirikiano wao."
Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu akitolewa katika Hospitali ya Nairobi nchini
Kenya kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa ajili ya safari
ya kuelekea nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.
0 Comments