Washtakiwa
wanne katika shauri la kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na
makosa la kimtandao wameachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mwanza kutupilia mbali hoja za kuzuia dhamana zao zilizowasilishwa na upande wa
Jamhuri.
Uamuzi huo
umetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Wilbert Chuma leo Desemba 15,
baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi, Mashaka Tuguta, Ogastini
Kulwa na Jebra Kambole kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka ni
dhaifu mbele ya macho ya sheria.
Washtakiwa
katika shauri hilo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza
wanaodaiwa kuvishana pete ya uchumba licha ya wote kuwa wanawake.
Wengine ni
Aneth Mkuki anadaiwa kufanikisha sherehe wawili hao kuvishana pete na Richard
Fabian anayeshtakiwa kwa kosa la mtandao kwa kusambaza video za tukio hilo
kwenye mitandao ya kijamii.
Katika
uamuzi wake, Hakimu Chuma amesema Mahakama haiwezi kufanyia kazi maelezo na
vitu vya mashaka na uvumi kuwa washtakiwa wanaweza kudhuriwa na jamii
iliyochukizwa na kitendo wanachoshtakiwa nacho.
“Ni uamuzi
wa Mahakama kuwa dhamana ni haki ya washtakiwa na upande wa mashtaka umeshindwa
kuwasilisha hoja za msingi kwa nini wanyimwe dhamana zaidi ya kutoa hoja za
hisia kuwa wakiachiwa watadhuriwa na jamii bila kueleza watadhurikaje na nani
haswa atawadhuru,” amesema Hakimu Chuma katika uamuzi wake
Washtakiwa
wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na
mdhamini mmoja mwenye kitambulisho na barua ya utambulisho kutoka mamlaka
inayotambulika kisheria pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh6 milioni.
Shauri limeahirishwa hadi Januari 8, mwakani.
0 Comments