Taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida inamshikilia mshindi
wa kwanza kura za maoni CCM jimbo la Singida kaskazini, Haider Hussein
Ghulamali (46), kwa tuhuma ya kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili taslimu
kwa afisa usalama wa taifa (jina tunalo).
Lengo la
Ghulamali mfanyabiashara na mmiliki wa kiwanda cha magodoro mjini Dodoma,ni
kwamba afisa usalama huyo amtolee taarifa nzuri Kwenye vikao vya ngazi za juu,
ili aweze kuthibitishwa na vikao hivyo, kuwa mgombea ubunge jimbo la Singida
kaskazini.
Mkuu wa
TAKUKURU mkoa wa Singida, Joshua Msuya, alisema Ghulamali amekamatwa Desemba 12
mwaka huu saa 8.30 mchana, maeneo ya Rafiki resort wakati akikabidhi rushwa
hiyo iliyokuwa imehifadhiwa kwenye bahasha.
Msuya
alisema desemba 11 mwaka huu,ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa vitendo
vya rushwa kwa mmoja wa wana CCM anayewania ubunge jimbo la Singida, ambaye ni
Ghulamali.
“Baada ya
kupokea taarifa hiyo uchunguzi ulianza ikiwa ni pamoja na kuchunguza vitendo
rushwa alivyofanya mtuhumiwa huyo, kabla na baada ya kura za maoni kupigwa
desemba 10 mwaka huu huko kijiji cha Ilongero.Kura hizo zilimpitisha Ghulamali
aliyepata kura 606 kati ya kura 1009 zilizopigwa,” alisema.
Mkuu huyo,
alisema baada ya zoezi hilo kupita la kura za maoni,mtuhumiwa kwa juhudi zake
aliweza kupata namba za simu za afisa wa usalama wa taifa ambaye walikuwa
hawafahamiani.
“Baada
kupata namba ya simu ya afisa usalama taifa, Ghulamali aliweza kumpigia na
akatoa maombi yake ya kusafishiwa taarifa kwenye vikao vya juu.Baada ya maombi
hayo,aliweza kutoa rushwa ya shilingi milioni mbili,na kumkabidhi afisa huyo.
Ndipo alipokamatwa na TAKUKURU waliokuwa wameweka mtengo,” alisema Msuya.
Alisema
uchunguzi zaidi bado unaendelea kuhusiana na mtuhumiwa Ghulamali kabla ya
uchaguzi na baada ya uchaguzi wa kura za maoni.
Mkuu huyo wa
TAKUKURU,ametoa rai kwa wanachama wa vyama vyote vya siasa,wagombea na wananchi
kwa ujumla, kuzingatia sheria za uchaguzi ndani ya vyama vyao.Pia kujiepusha na
vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi ndani vyama.
“TAKUKURU
itamkamata mgombea,mpambe na mwanachama yeyote atakayejihusisha na vitendo ya
kuomba na kupokea rushwa,na ikipata ushahidi wa kutosha,itamfikisha mhusika
mahakamani,” alisema Msuya.
0 Comments