Serikali
imekifungia Kiwanda cha kukamua mafuta cha Alizeti Mount Meru Millers Ltd muda
usiojulikana kwa madai ya kukaidi agizo la kulipa faini ya Sh20milioni.
Uamuzi wa
kukifunga kiwanda hicho umetolewa Jumatano na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira ,Kangi Lugola alipokuwa
kwenye kwanda hicho kilichopo kijiji cha Manguanjuki Manispaa ya Singida.
Kabla ya
kutoa uamuzi huo mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Singida,
Lugola alisema Novemba 29 mwaka jana, mtangulizi wake Luhaga Mpina, aliuagiza
uongozi wa kiwanda hicho ulipe faini ya Sh20milioni kwa kosa la kutiririsha
maji taka yenye kemikali kwenye makazi ya watu .
“Maji taka
yameelekezwa kwenye makazi ya wananchi wanaokizunguka kiwanda .Pia maji hayo
yenye kemikali, yameelekezwa kwenye ziwa la Singidani lenye viumbe hai wakiwemo
samaki. lakini hadi leo, agizo la Waziri Mpina, halijatekelezwa’’ amesema
Lugola na kuongeza kwamba
‘’Kutokana
na ukiukwaji wa sheria za mazingira, Mpina alikipa adhabu ya kulipa faini
Sh20milioni ambayo haijalipwa hadi leo”, amesema Waziri Lugola kwa masikitiko.
Lugola
amesema kwamba kiwanda hicho kimetekeleza agizo la kununua mashine ya kutibu
maji taka, lakini maji taka hayo, hayajaelekezwa kwenye mashine hiyo.
“Maji hayo
yenye kemikali bado yameendelea kuwa kero kwa wananchi hadi leo, na yanaathiri
viumbe hai vilivyopo kwenye ziwa Singidani. Hii dharau kwa serikali
haikubaliki”, amesema
Naibu waziri
huyo, amesema wananchi wanaozunguka kiwanda hicho wamekuwa wakitoa kilio chao
serikalini kwa miaka minne, kwamba wanaathiriwa na maji yenye kemikali na moshi
mnene wa kiwanda cha Maount Meru.
“Binafsi leo
nimefika kwenye kiwanda hiki na baada ya kufanya ukaguzi wa kina, nakiri kwamba
kilio cha wananchi wa Manguanjuki ni cha kweli na kinahitaji tiba ya kudumu.
Mkuu wa wilaya ya Singida, naagiza kuanzia sasa, usimamie kufungwa kwa kiwanda
hiki”,amesema na kuongeza;
“OCD pia
nakuagiza uwatafute Wakurugenzi wa kiwanda hiki Atul Nittal, Arvind Mittal na
Tarsem Aggarwal, popote walipo na kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya
sheria kwa kukaidi agizo la Serikali”.
Kwa upande
wake meneja Uhusiano, Nelson Mwakambuta, amesema kiwanda hicho kimekuwa
kikifanyiwa ukaguzi mara kwa mara na mamlaka mbalimbali. Lakini wamekuwa
wakiaambiwa na viongozi hao kuwa kiwanda hicho, hakina tatizo lolote
linalohusiana na kwenda kinyume na sheria za mazingira.
“Kufungwa
kwa muda usiojulikana kwa kiwanda hiki, kutaathiri ustawi wa watumishi wengi wa
kiwanda na familia zao. Pia wakulima wa zao la alizeti ndani na nje ya mkoa wa
Singida, nao watakuwa wamepata pigo. Hatupingani na serikali tutatekeleza yale
yote tuliyoagizwa”,amesema meneja huyo.
0 Comments