Hali ya
sintofahamu imejitokeza katika jiji la Harare baada ya vifaru kuonekana
vikielekea mjini ambako vilitumika kufunga barabara kubwa za kuingia na kutoka
nje.
Aidha vyombo
vya habari vya ndani vimeripoti kwamba msafara mkubwa wa wanajeshi wenye silaha
ulizingira kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ZBC. Kadhalika
Shirika la Reuters limesema vifaru vinne vilionekana mitaani.
Baadhi ya
watu walianza kusambaza picha za magari ya kijeshi kwenye mitandao ya kijamii.
Baadhi walisema (mapinduzi) lakini gazeti la Independent la Uingereza
limeshindwa kuthibitisha ukweli wa picha hizo na msafara wa magari hayo ya
kijeshi.
Hata hivyo,
tukio hilo limekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi Jenerali Constantino
Chiwenga kutishia kuingilia kati na akaagiza “kusitishwa” mara moja ufukuzaji
wanachama kutoka chama cha Zanu PF cha Rais Robert Mugabe kufuatia kufutwa kazi
kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.
Jenerali
Chiwenga akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na
walau makamanda 90 wa ngazi ya juu kwenye makao makuu ya jeshi, Jumatatu
alisema: "Ufukuzaji huu unaolenga wanachama wa chama wenye uhusiano na
harakati za ukombozi lazima ukome mara moja."
Ripoti
zinasema kwamba jeshi limekuwa likimuunga mkono Mnangagwa kumrithi Mugabe, 93,
lakini mke wa mzee huyo Grace ameibuka na kuwa mshindani mwenye nafasi kubwa.
Mnangagwa
alifukuzwa serikalini na kwenye chama wiki iliyopita baada ya kushutumiwa
kwamba alikuwa anapanga njama za kumwondoa mamlakani Mugabe. Mnangagwa
amekimbilia uhamishoni.
Waziri wa
Elimu ya Ufundi Jonathan Moyo amemkemea Jenerali Chiwenga lakini umoja wa
vijana wa Zanu PF umesema “uko tayari kufa” ili kuitetea serikali ya Rais
Robert Mugabe.
"Sisi
kama vijana wa Zanu-PF ni simba aliyesimama imara na mwenye sauti, kwa hiyo
hatutalemaa na kukunja mikono yetu wakati vitisho vikitolewa dhidi ya
Mugabe," ilisema taarifa ya Katibu mkuu wa vijana wa Zanu-PF Kudzai
Chipanga.
0 Comments