Kwa mara ya
kwanza, Tundu Lissu amezungumzia shambulio la kinyama alilofanyiwa na watu
wasiojulikana kwa kueleza kuwa, alinusurika kufumuliwa fuvu la kichwa kwa
risasi.
Lissu,
Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS), aliyasema hayo jana, jijini Nairobi anakotibiwa
wakati akihojiwa na Jarida la Financial Times la Uingereza.
Yakiwa ni
mahojiano yake ya kwanza tangu aliposhambuliwa nje ya makazi yake yaliyoko Area
D, mjini Dodoma Septemba mwaka huu, Lissu mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali
alisema anaamini alikuwa mlengwa wa jaribio la mauaji.
Akizungumzia
shambulio hilo dhidi yake, alisema sekunde chache baada ya watu wawili wenye
silaha kushuka katika gari lililokuwa likimfuatilia kwa wiki tatu, derava wake
alimsukuma chini ya sakafu ya gari lake wakati wakihangaika kukwepa risasi
nyingi zilizoelekezwa kwenye gari lake, nyingi zilimpiga mgongoni na nyingine
kwenye bega lakini risasi moja ilikosakosa kufumua fuvu lake la kichwa.
“Hali ikawa
mbaya sana kwa sababu sikuweza kuhesabu risasi, naambiwa kwamba risasi 38
zilipiga gari langu na 16 zilinipata na moja iliyokuwa imelengwa kunifumua fuvu
la kichwa ilinipiga begeni karibu na shingo,” alikaririwa Lissu.
Mwanasiasa
huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa kambi ya upinzani
alikakririwa akieleza zaidi kuwa kilichotokea ni ushahidi wa kile ambacho
amekuwa akikizungumzia mara nyingi kuhusu uwepo wa watu waovu wanaotekeleza
kampeni ovu ya kuipeleka nchi pabaya.
Wakati Lissu
akikutwa na mkasa huo mbaya, historia yake ya kisiasa inaonyesha kuwa
amekwishtakiwa mara sita, mwaka huu kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya
uchochezi.
Wachambuzi
na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa shambulio hilo linaweza kuwa
moja ya mikakati ya magenge ya wapinzani wa serikali waliobanwa na dola ambao
sasa wanajaribu kutumia kila aina ya mbinu kuifarakanisha jamii hususan
wanasiasa.
Tayari Jeshi
la Polisi limekwishaanzisha uchunguzi wa tukio hilo na Inspekta Jenerali (IGP),
Simon Sirro amekwitoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia
uchunguzi huo kuzitoa kwa makachero wa polisi.
Sambamba na
hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas naye alikutana na waandishi wa
habari kuzungumzia tukio hilo ambapo alitoa rai kuwa shambulio hilo
lisichukuliwe kisiasa kwa sababu ni uhalifu wenye sura za ile ile ya matukio ya
kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini.
Katika
mkutano wake na wanahabari alioufanya siku chache baada ya Lissu kushambuliwa,
Dk. Abbas alionya kuhusu upotoshaji uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watu
waliokuwa wakijaribu kuipata matope serikali kwa kuihusisha na shambulio na
aliwataka wote wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi, akiwemo Lissu kutoa
ushirikiano kwa polisi.
0 Comments