Aliyekuwa
mwanachama CCM, ambaye baadaye alihamia Chadema, Lawrance Masha amejivua
uanachama katika chama hicho akidai upinzani wa sasa umeridhika na hali ya
kuendelea kuwa wakosoaji ili kukisaidia chama tawala kujirekebisha.
Pia amesema,
“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa upinzani wa sasa nchini hauna nia wala sababu
ya kutafuta fursa ya kuunda Serikali kupitia falsafa, sera na uongozi mbadala.”
Masha
ameeleza hayo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa leo Jumanne
Novemba 14.
Masha ambaye
aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, katika Serikali ya awamu nne,
amesema upinzani hauwezi kutegemea kushika dola kwa kutegemea madhaifu ya CCM
badala uwezo wake kama mbadala.
Amesema kazi
kubwa ya chama chochote cha siasa ni kujiandaa na hatimaye kushinda uchaguzi
ili uweze kuunda na kuendesha Serikali na dola kama njia ya maono yaliyo kwenye
ilani ya uchaguzi kwa lengo la kuleta maendeleo na ustawi katika nchi.
“Nilijivua
uanachama CCM mwaka 2015 na kujiunga Chadema nikiamini nitashiriki kukifanya chama
hiki kikomae na kufikia hatua ya kuwa mbadala kifalsafa, kisera na uongozi.
Hata hivyo uzoefu wangu wa miaka miwili ndani ya Chadema umenionyesha chama
hiki kina safari ndefu kisiasa na kuwa chama mbadala cha kuunda Serikali.
“Mpaka sasa
chama hiki kimendelee kujikita katika kukosoa na kuonyesha madhaifu ya Serikali
hasa Rais John Magufuli binafsi. Natambua kwamba kukosoa ni kazi muhimu ya
chama cha upinzani, kazi hii haikifanyi chama kuwa mbadala cha kuunda
Serikali,”amesema Masha katika taarifa hiyo.
Masha ambaye
aliwani kuwa Mbunge wa Nyamagama mwaka 2005-10, amesema siyo sahihi kwa vyama
vya upinzani kuwekeza katika kumpinga Rais Magufuli ambaye ni mkuu wa nchi
pekee anayetekeleza kwa vitendo mambo ambayo upinzani ilikuwa ikiyapigia kelele
kwa miaka mingi, na kuwashinda viongozi wa CCM waliomtangulia.
“Nimejivua
uanachama kuanzia leo, nina imani uamuzi huu utanipa fursa ya kutafakari kwa
kina safari yangu ya kisiasa ndani ya nchi hii. Nawashukuru viongozi wa Chadema
kwa miaka miwili ya kufanya kazi pamoja nao nawatakiwa kila la kheri,” amesema
Masha ambaye alikuwa ni miongoni mwa watu walioshirikia kampeni za uchaguzi za
mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
0 Comments