Kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa jana Septemba 20,2017 la kujengwa uzio machimbo ya Tanzanite Mererani kwa kuliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujenga uzio wa kuzunguka vitalu vya kuanzia A hadi D vyenye madini ya Tanzanite katika eneo Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ili kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo, mapema leo Septemba 21, Jeshi hilo limeanza kutekeleza maagizo hayo.
JWTZ
tayari kupitia Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuyo ametua Mererani
kwa helkopta na kukagua maeneo ambayo ukuta utaanza kujengwa mara moja huku
Wachimbaji na wananchi wakifurahia kuanza kwa zoezi hilo na wameahidi ushirikiano.
Agizo la Rais Magufuli alilitoa
wakati wa sherehe ya ufunguzi wa barabara ya Kia – Mererani iliyofanyika katika
eneo la Mererani, yenye KM 26.
Katika maagizo yake hayo, Mhe. Rais
Magufuli alieleza kuwa, pamoja na kujenga uzio huo haraka iwezekanavyo, soko la
Tanzanite litapaswa kuwa katika eneo hilo, Tanzanite yote itapita kupitia lango
moja na ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kushiriki katika ununuzi wa
Tanzanite.
“Lile eneo la kitalu kuanzia A hadi D
ambalo ndio lina mali nyingi ya Tanzanite, naagiza Jeshi la Wananchi kupitia
Suma-JKT na wengine, najua wameshamaliza utafiti, waanze kujenga ukuta eneo
hilo lote na kazi hii ifanyike haraka, watakapojenga ukuta wataweka kamera na
patakuwa na mlango mmoja ambapo patajengwa vifaa maalum, nataka niwaeleze
ukweli ndugu zangu wa Simanjiro hata kama utameza Tanzanite itaonekana”
alisema Mhe. Rais Magufuli huku
akivipongeza vyombo vya ulinzi na
usalama kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa kukabiliana na wizi wa madini ya
Tanzanite na ameitaka kamati inayoongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba Prof.
Palamagamba John Kabudi kuanza kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na wananchi
kuhusu uchimbaji na biashara ya madini hayo ili mchakato wa kurekebisha
mikataba ufanyike.
“Ripoti ya kamati iliyoundwa na Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai imeonesha kuwa
Serikali na wananchi tunanufaika kwa asilimia 5 tu ya madini haya ya Tanzanite,
zinazobaki zote wananufaika watu wengine, hii haiwezekani ni lazima tuwe na
mikataba itakayotunufaisha na sisi, haiwezekani Tanzanite tunayo sisi tu lakini
tunapata asilimia 5, halafu hapa Mererani hakuna maji na hakuna gari ya
wagonjwa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli
amewaahidi wananchi wa Mererani kuwa atawapelekea gari la wagonjwa na pia
atalifanyia kazi tatizo la uhaba wa maji linawakabili wananchi hao.
Meja Jenerali Michael Isamuhyo
akitembelea na kuoneshwa eneo la vitalu A mpaka D katika eneo la machimbo ya
Tanzanite Mererani wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara leo Septemba 21, 2017,
tayari kwa kuanza kazi ya kujenga uzio kuzunguka eneo hilo kufuatia amri ya
Rais Dkt John Pombe Magufuli aliyotoa jana ili kudhibiti biashara ya madini
hayo yanayopatikana Tanzania pekee. Picha na mpiga picha wetu.
0 Comments