Mradi
wa afya ya macho katika mikoa ya Morogoro na Singida umeonyesha kuwa kuna
uwezekano wa kuepuka upofu unao zuilika nchini Tanzania.
Mnamo
2022, ilikadiriwa kuwa watu milioni 8.2 nchini walipoteza uoni na bila juhudi
za makusudi, idadi hii inaweza kuongezeka (ripoti ya IAPB, 2020).
Boresha
Macho, ni mradi wa afya ya macho uliosimamiwa na Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Sightsavers, uliolenga kurejesha na kulinda uoni kwa kutoa huduma
ya afya macho kwa makundi yote yakiwemo, wazee, watu wenye ulemavu na wasio na
ulemavu.
Ukifadhiliwa
na serikali ya Uingereza kupitia UK Aid Match na kutekelezwa na Sightsavers kwa
ushirikiano na Wizara ya Afya ya Tanzania, mpango huo ulisaidia zaidi ya watu
178,000 kupata huduma za msingi za afya ya macho. Aidha, mradi huo ulilenga
hasa watu wenye ulemavu na wanawake, ambao kwa kawaida hukabiliwa na vikwazo
vya kupata huduma za afya japokuwa hawapaswi kuachwa nyuma.
Mradi
huo umebadilisha maisha ya watu kama Bibi Holo kutoka mkoani Singida ambaye
anaweza kulima na kutunza wajukuu zake. Kupoteza uoni kutokana na mtoto wa
jicho kulifanya kazi hizi kuwa ngumu na Holo alihisi kutokuwa na nguvu kwenye
miguu yake.
Upasuaji
wa mtoto wa jicho umempa "mwanzo mpya". Anahisi furaha, nguvu, na
anaweza kufanya kazi na kutembea tena. Holo sasa amemuhamasisha kaka yake pia
kutafuta matibabu kwa tatizo lake la uoni.
Edwin
Maleko, Meneja Programu wa Sightsavers, anasema: “Upatikanaji wa huduma za afya
ya macho ni haki ya msingi ya binadamu na afya ya macho bora ni sawa na fursa,
kuruhusu watoto kujifunza na watu wazima kufanya shughuli za kujipatia riziki.
Kuzingatia
afya ya macho ni sehemu muhimu katika kuleta mwamko katika elimu, ustawi wa
jamii, uchumi na matokeo ya afya bora. Ambayo hatimaye husaidia kupunguza
umaskini na kutoa fursa kwa watu binafsi, jamii na taifa kustawi.”
Upatikanaji
wa huduma ya macho uliboreshwa kupitia mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
•
Upasuaji wa mtoto wa jicho kwa zaidi ya watu 17,000 na utoaji wa miwani kwa
zaidi ya watu ,7000
•
Uchunguzi katika jamii kwa njia ya huduma ya mkoba/kliniki tembezi. Mafunzo ya
kitaalamu kwa wahudumu wa afya ya macho
•
Ukaguzi na uboreshaji wa upatikanaji wa huduma katika vituo vya afya
•
Mafunzo jumuishi ya ulemavu na ushirikishwaji wa kijinsia kwa wataalamu wa afya
•Kuongeza
uelewa kwa kushirikiana na mashirika ya wanawake na watu wenye ulemavu.
Edwin
anaendelea kwa kusema: “Tunaihimiza serikali na wadau wengine kuendelea
kuboresha huduma za afya ya macho na mafunzo ya kitaaluma. Aidha, kujumuisha
huduma ya macho katika mifumo ya elimu ili kukabiliana na afya ya macho ya
mtoto, na kufanya kazi kwa karibu na mashirika ya wanawake na watu wenye
ulemavu ili kuhakikisha huduma zinabaki kuwa jumuishi.
Mradi
wa Boresha Macho uliwezekana kutokana na msaada mkubwa kutoka serikali ya
Uingereza katika kampeni ya kuchangisha pesa ya Sightsavers 'End is in Sight'.
Ilianza kutumika kuanzia Oktoba 2019 mpaka Disemba 2022 na iliweka misingi
imara ambayo serikali na washirika sasa wanaitumia. Bajeti za afya na
rasilimali tayari zimeongezwa na Sightsavers kwa sasa inasaidia mapitio ya
mitaala ya mafunzo ya kitaaluma.
0 Comments