Rais wa
Marekani Donald Trump amesema kuwa nchi yake imejipanga na iko tayari
kuishambulia tena Syria kama itarudia kufanya mashambulizi ya silaha za
kemikali.
Onyo hilo la
Trump limekuja baada ya Marekani, Ufaransa na Uingereza kufanya mashambulizi
katika maeneo matatu ya Syria ndani ya saa 12, kwa kufyatua makombora 100.
Marekani na
washirika wake hao wanadai kuwa Syria ilifanya mashambulizi ya silaha za
kemikali wiki iliyopita katika eneo la Douma na kusababisha vifo vya watu wasio
na hatia, kinyume cha sheria za kimataifa.
Urusi ambao
ni washirika wa Syria waliwasilisha hoja katika Baraza Kuu la Usalama la Umoja
wa Mataifa ikitaka kitendo kilichofanywa na Marekani kulaaniwa vikali na umoja
huo, ombi ambalo lilipingwa baada ya mjadala wa muda mrefu uliokuwa na maneno
makali, kwa mujibu wa ripoti.
Balozi wa
Urusi kwa Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia alisoma nukuu ya maneno ya Rais
Vladimir Putin kwa kutekeleza mashambulizi hayo bila kuzingatia sheria za umoja
wa mataifa na bila kusubiri majibu ya shirika la upelelezi la umoja wa mataifa
linaloshughulikia silaha za kemikali la OPCW.
Wajumbe wa
OPCW wanatarajia kuzulu eneo la Douma wiki ijayo kufanya uchunguzi wa tuhuma za
Syria kutumia silaha za kemikali.
Syria
imekana kutumia silaha hizo na kueleza kuwa tukio hilo limefanywa na waasi kwa
lengo la kuichonganisha serikali ya Syria na wananchi wake pamoja na jumuiya za
umoja wa mataifa. Rais Bashar Al-Assad ameseam kuwa mashambulizi ya Marekani
yanazidi kumuimarisha.
0 Comments