Afya ya
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye anaendelea na
matibabu nchini Ubelgiji, inazidi kuimarika na sasa anaweza kufanya mambo mengi
mwenyewe ikiwamo kwenda kuoga na kutembea kwa kutumia magongo.
Lissu ambaye
pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), alipelekwa Ubelgiji
Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alipokuwa akipatiwa
matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.
Mbunge huyo
aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana
nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano kati ya hizo zikimpata
katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Vinceti
Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema jana kuwa Lissu ameanza kutembea
mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali ikiwemo kwenda
kuoga bila msaada wa mtu mwingine.
"Tunamshukuru
Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri... tangu ameanza kupatiwa matibabu na
mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno," alisema na kueleza
zaidi:
"Maendeleo
ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza
kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa maliwatoni lakini
sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia mguu chini.
"Anakula
mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo
makubwa."
Mghwai
alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo ikawa
sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa matibabu na
bila usumbufu wowote.
Alisema
Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa Hospitali
ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu waliokuwa wakienda
kumjulia hali.
"Kwa
sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari wanamfanyia
mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona na ndiyo sababu
anaendelea kupona haraka," alisema Mghwai.
"Ubelgiji
muda wote yuko na madaktari akipatiwa matibabu hasa mazoezi ya viungo... huku
ni kazi kazi tu. Na madaktari waliahidi kufanya kazi.
"Kule
Nairobi wakati mwingine alikuwa akiwaambia madaktari wamuache pale anaposikia
maumivu wakati wa mazoezi lakini sasa hakuna kitu kama hicho na wamemwambia
avumilie apone."
Kuhusu
risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji
hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na madhara
kwake kiafya.
"Kule
Ubelgiji kazi kubwa ni kumfanyisha mazoezi ili sasa aweze kurejea katika hali
yake na ndicho ambacho wanaendelea nacho na kwa kweli tumeanza kuona maendeleo
makubwa."
Kuhusu
gharama za matibabu, Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100 zinatumika kila
mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge halijatoa fedha na familia
inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa huku na kule.
Alisema
fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na wadau
mbalimbali na wamekuwa wakifanya harambee kadhaa za kuchangia.
"Gharama
ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali hiyo na
kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi ni fedha za
matibabu pekee," alisema Mghwai.
Alieleza
zaidi kuwa fedha zilizochangwa hazitoshi kumtibu Lissu na kwamba kwa sasa wadau
wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali inagharamia matibabu
yake.
Alisema
familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha
matibabu yake.
"Tunaamini
hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa
mzima."
Alisema
gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya matibabu ya
Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na si yeye peke yake
kuzungumzia.
Lissu ambaye
Januari 6 alizungumza na waandishi wa habari akiwa nje ya Hospitali ya Nairobi,
ikiwa ni siku moja kabla ya kusafiri kuelekea nchini Ubelgiji, alieleza kuwa
alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na 16 zilimjeruhi maeneo mbalimbali ya
miguu, mikononi na kwenye nyonga.
Lissu
alisema kutokana na shambulio hilo alifanyiwa operesheni 17 zilizofanikisha
kuondoa risasi saba zilizoingia mwilini huku risasi moja ikisalia.
Wataalam wa
afya walimshauri kuiacha risasi hiyo iliyopo kwenye nyonga wakisema kuwa
inaweza kuleta madhara zaidi kama watajaribu kuitoa.
0 Comments