Vigogo wa
Chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (Shirecu), wa Chama cha Ushirika mkoa wa
Mwanza (Nyanza) wameponea chupuchupu kuwekwa ndani na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa kutokana na kutajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliohusika kuuza mali
za ushirika.
Akizungumza
kwenye mkutano wa wadau wa zao la pamba uliojumuisha mikoa 16 ya Tanzania bara
jana Desemba 22, Waziri Majaliwa alitaka kumuiagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Shinyanga, Simon Haule kuwakamata vigogo hao.
Hata hivyo,
aliwapa muda hadi Januari 13, mwakani wafike ofisini wake wakiwa na nyaraka
zinazoonyesha mali za ushirika zilipo.
Alisema
wamepoteza mali nyingi kwenye ushirika wa Nyanza likiwemo jengo la usafirishaji
na viwanja ambavyo vimechukuliwa na watu wasio wanachama.
Alisisitiza
kuwa watakapofika ofisi kwake wawe na maelezo kamili ya zilipo mali hizo, kama
ziliuzwa waliouziwa wafike na nyaraka zinazoonyesha waliuziwa na nani.
“Nilitaka
kumwambia RPC aondoke na nyinyi lakini ninawapa nafasi kila mmoja aje na
maelezo ya zilipo mali na kama zimeuzwa hao waliouza waseme waliuziwa na nani,"
alisema na kuongeza,
"Tukutane
siku hiyo ofisini kwangu saa 3 asubuhi. Lazima tuhakikishe mali hizi
zinapatikana ili ushirika uendelee kuwa imara."
Miongoni mwa
vigogo hao zaidi ya 13, wamo waliokuwa wahasibu ambapo upande wa Shirecu yumo
pia meneja wake wa mkoa, Joseph Mihangwa na James Kusekwa.
Majaliwa
alisema Shirecu inadaiwa Sh11 bilioni walizokopa Benki ya TIB pamoja na Sh 1.2
bilioni wanazodaiwa na wafanyakazi.
0 Comments