Katika
makala hii tutaangalia mafundisho yanayohusiana na kile wanachokiita “Roho za
Kimaeneo”. Kulingana na mafundisho hayo, wanadai kuna roho chafu maalum ambazo
zinatawala jamii, vijiji, miji, jiji au hata nchi nzima. Hiyo ina maana kwamba,
roho hizo zinatawala katika eneo zima kulingana na jiografia ya eneo lenyewe;
na hivyo huitwa “Roho za Maeneo”. Inaendelea kufundishwa zaidi kwamba eti hizi
roho za maeneo zanao uwezo na mamlaka ya kuwabana watu katika giza, vifungo na
dhambi kulingana na jiografia ya eneo lao. Kimsingi, zaidi ya hilo, hawa
wanaohamasisha mafundisho hayo, wanatuambia kwamba hizi roho za maeneo zinao
uwezo wa kushikilia jamii ndogo au miji kiasi kwamba Injili peke yake haiwezi
kufaa, kupata kuingia wala kupendwa au kuenea katika eneo hilo hadi hapo hizi
roho za kimaeneo zitakapotambulikana na kisha zikafungwa, zikazidiwa nguvu
pamoja na kukemewa kwa njia ya maombi. Wanafundisha kwamba watu hawawezi kumjia
Bwana, wakaokolewa na kukombolewa kutoka katika dhambi, giza, pamoja na vifungo
mbalimbali, kwa idadi kubwa mpaka kwanza hapo tutakapotambua na kisha kuzifunga
na kukemea nguvu za roho hizo za kimaeneo. Hivyo ndivyo wanavyosema na
kuwafundisha watu.
Hiki ndicho
kidokezo cha mafundisho yao kwa lugha rahisi kadiri iwezekanavyo, na nina
hakika kwamba utakubali kuwa ikiwa mafundisho haya ni ya kweli, basi ni ya
umuhimu mkubwa. Kuenea kwa Injili pamoja na kuokolewa kwa watu kunategemea
ufahamu na matumizi ya mafundisho haya, ikiwa mafundisho hayo ni ya kweli!
Jambo hili haliwezi kuwa swala la jinsi mtu aonavyo au tafsiri ya kibinafsi,
kwa sababu litaathiri ufahamu wetu kuhusiana na jinsi Injili ilivyo, pamoja na
lile alilolifanya Yesu pale Kalvari.
Kama ilivyo
katika zile makala nyingine zilizopita, napenda kwanza niangalie yale ambayo
Maandiko yanavyosema na kufundisha. Kwa hivyo, kwa muda huu, hatutaangalia
Maandiko ambayo watu wanadhani wamepata kuyaona mambo hayo yakifundishwa. Jambo
hili ni la msingi na lenye uzito mkubwa kiasi kwamba hatuwezi kuyaachia kwenye
ubunifu au hisia za kibinadamu tu. Tunachotafuta ni maandiko ambayo mambo haya
yanafundishwa dhahiri na kutajwa bayana.
Mambo haya
yanafundishwa wapi ndani ya Agano Jipya?
Kwa jibu la
urahisi na la ujumla kuhusiana na habari hiyo hapo juu ni – “Hakuna popote!”
Hatuyapati mahala popote katika Agano jipya, mafundisho haya yahusuyo kutambua
na kuzifunga roho za kieneo!
Yesu
hakutumia au kufundisha mbinu hii.
Hakuna
mahali popote tunaposoma kuwa Yesu aliibainisha roho iliyokuwa ikitawala eneo,
kijiji au mji, na kisha akaifunga na kuikemea kabla hajaanza kuhubiri na
kufanya miujiza mahali hapo.
Hakuna
mahali popote ambapo Yesu aliwafundisha mitume wake au mtu mwingine yeyote
kwamba Neno la Mungu linaweza kuwa na nguvu na mafanikio katika eneo fulani
ikiwa kwanza utaibainisha roho ya lile eneo na kuifunga na kuzishinda nguvu
zake kwa njia ya maombi. Kamwe hatusomi popote Yesu akiitumia au kuifundisha
mbinu hii.
Mitume hawakutumia au kufundisha mbinu hii.
Hakuna
mahali popote pale katika Injili au kwenye Matendo ya Mitume ambapo tunasoma
habari za mitume au mtu mwingine yoyote yule akitumia mbinu za jinsi hiyo
katika kuineza Injili. Mtume Paulo alitembelea miji mingi sana ambamo kulikuwa
na zinaa ya kutisha, mambo ya kimwili, uchawi pamoja na dhambi. Hakuna popote
pale ambapo tunasoma juu yake akizitambua kwanza roho hizo katika miji hiyo ili
aone ni aina gani ya roho za kimaeneo zinazotawala katika miji, wala hatusomi
mahala popote pale na kuona akiomba juu ya roho za aina hiyo ili kwamba kazi ya
Injili ipate kustawi.
Hakuna
mahali popote pale ndani ya maandishi yao kwa makanisa au kwa watu binafsi,
ambapo mitume hawa wamepata kutaja tu mbinu za jinsi hiyo, licha ya
kuzifundisha. Yapo mahusia mbalimbali kwa ajili ya kuomba katika Agano Jipya.
Lakini hakuna mahali popote pale ambapo mitume wanaelekeza kuwa roho za
kimaeneo zina uwezo juu ya watu katika baadhi ya maeneo na kwamba watu hawana
budi kuomba dhidi ya roho hizo na kuzivunja nguvu zake, ili kwamba Injili ipate
kustawi na ili wanawake na wanaume wapate kuokolewa.
Hayapo
mafundisho ya jinsi hiyo ndani ya Agano Jipya. Kwa msingi huu pekee, tunaweza,
kwa usalama kabisa, kuyakataa mafundisho ya jinsi hii.
Lakini sasa,
mtindo wa jinsi hii haufudishwi kwenye Agano la Kale wala hatuna hata mfano
mmoja katika Agano la Kale, unaoelezea juu ya mtu yeyote anayezitambua roho za
kimaeneo na kufunga nguvu zake kabla kazi ya Bwana haijakamilishwa ipasavyo.
Kwa kweli, waandishi hao wa kisasa wanarejea katika maandishi fulani fulani ya
Agano la Kale, na tutakwenda kuangalia maandishi hayo baadaye, lakini hata
hivyo, hakuna hata andiko moja linalounga mkono mtindo huo na mbinu zao
zinazoenezwa na waandishi hao.
Jukumu la
Uongo
Wanawezaje
walimu hawa wa siku hizi kusema, “Lazima uzitumie mbinu hizi ili kuhakikisha
mafanikio ya uInjilisti katika ulimwengu”, wakati ambapo maandiko hayatushauri
kufanya hivyo? Wanaweka jukumu juu ya watu we Mungu wakati ambapo maandiko
hayaweki jukumu la jinsi hiyo. Kwa maneno mengine, wao huongezea maneno yao juu
ya Neno la Mungu – na wakizitumia mamlaka zao juu ya watu wa Mungu, mamlaka
ambazo hazitokani na Mungu. Hili ni jambo la hatari sana. Ni jambo moja kusema
kuwa, kwa sababu maandiko hayawazuii kuzitumia mbinu hizo, kwa hivyo wao
wanajisikia uhuru kuzitumia. (Hata hivyo, hoja hii si ya msingi, kwa sababu
mafundisho yao yanagusa kweli za msingi za Injili na ufanisi katika kuenezwa
kwake, hivyo wanapaswa kuonyesha kwa uhakika mambo hayo yanafundishwa wapi
katika maandiko, kabla hawajafundisha na kuzitumia kanuni hizo). Lakini kwa
kweli wanafundisha kanuni zao za lazima kwa ajili ya kueneza Injili. Huo ni
udanganyifu na unaweza kuwapelekea watu wa Mungu, kutumbukia katika
kuchanganyikiwa, vifungo pamoja na hatari iwapo watapokea na kuyafuata
mafundisho ya jinsi hii.
Ikiwa mbinu
hizi za kuzitambua na kuzifunga roho za kimaeneo ni za lazima kwa ajili ya
kuleta mafanikio ya uenezaji wa Injili, kwa nini basi Yesu pamoja na mitume
wake hawakufundisha wala kutufunulia mambo hayo? Tunaelezwa na hawa walimu wa
kisasa kwamba maombezi dhidi ya mamlaka na uweza juu ya maeneo ya kijiografia,
yanahitajika sana kabla Injili haijapenya katika maeneo hayo. Je, mitume
walikuwa ni wajinga juu ya mbinu hizo? Au labda walishindwa kutufunulia kile
kilicho cha lazima kwa ajili ya uenezi wa Injili, na kwa ajili ya wokovu wa
nafsi za watu? Je kanisa litakuwa limeondolewa ukweli huu wa lazima kwa muda wa
miaka 2000? Hapana! Kanisa halijanyimwa ukweli huu wa lazima, na bado Injili
imeendelea kuenea muda wote huo kwa karne zote hizo, kama Yesu alivyosema
Injili haina budi kuenea, hata bila kanisa kufundisha au kuzitumia mbinu hizo
ambazo hawa walimu wa kisasa wamezibuni. Kutokea muda wa Matendo ya Mitume hadi
kufikia siku hii ya leo, kumekuwepo na uamsho, maelfu ya watu wamerejea kwa
Bwana kwa idadi kubwa, nao wameokolewa kutokana na dhambi, giza na vifungo vya
shetani pasipo hata kujulikana kwa mbinu hizo, kufundishwa wala kuzitumia!
Kutamani
“matokeo” kupita kiasi.
Lakini moja
ya kusudio lao kuu hawa wahubiri na walimu wa kisasa ni kuona “matokeo”. Mmoja
wa viongozi wa kanisa ambaye anaamini katika kutumia kanuni hizo amesikika
akisema kuwa iwapo kanisa lake halitaongezeka kutoka washirika 1000 hadi
kufikia washiriki 2000 ndani ya miaka miwili, basi hapo itakuwa ni kutokana na
kushindwa kwao katika kujaribu kwa makini kufanya hivyo. Kwa maneno mengine,
iwapo tutazitumia mbinu halisi basi tutegemee kanisani washirika kuongezeka
mara mbili zaidi ndani ya miaka miwili! Watu hawa wanalifanya kanisa kuwa kana
kwamba ni aina fulani ya biashara ambapo tunapaswa kuzitafuta kanuni bora zaidi
ili kutoa matokeo na kufikia malengo. Hata makanisa mengi kwa sasa yameanza
kutoa “maelezo ya umisheni” pamoja na malengo yao kwa ajili ya mafanikio yao.
Mtindo wa aina hii kwa kazi ya Mungu, umeazimwa moja kwa moja kutoka kwa
ulimwengu wa kibiashara. Hii yote inamdhalilisha Yesu Kristo ambaye ndiye
kichwa cha kanisa lake ambaye ndiye aliyetuonyesha kwa neno lake jinsi
itupasavyo kujishughulisha wenyewe. Mmoja wao amesema kwa uwazi kabisa kwamba
wanavutiwa zaidi na yale “yanayofanya kazi” ( yaani, yanayoleta mafanikio au
matokeo ) kuliko “yale yaliyo ya kweli”. Kwa hiyo basi, tayari wameanza kujenga
msingi wa udanganyifu wao. Katika kujiondoa kwao kutoka katika miongozo iliyo
sahihi ya Neno la Mungu, wao wamekuwa wakijiweka wazi kwa udanganyifu wa
shetani; kadiri wanavyoendelea na kuzitumia mbinu na kanuni zinazoweza
kuwaletea matokeo ya haraka na yenye kuvutia.
Yesu anaomba
kwa Baba akisema “Neno lako ni kweli”, Yohana17:17. Sasa kama watu wa Mungu,
sote tunatamani na kuomba kwamba Injili iweze kufikia na kuokoa nafsi za watu
wengi watuzungukao na ulimwenguni kote. Lakini watu wa Mungu, maombi yetu, kazi
zetu, pamoja na mafundisho yetu lazima yawe kulingana na neno la Mungu, ambako
ndiyo kweli. Hamu yetu ya “kuona matokeo” isituongoze kuelekea kwenye kuikataa
au kujitenga na Neno la Mungu kama lilivyofunuliwa katika maandiko; au
kuanzisha mbinu zetu wenyewe au mtindo wa fikra kwa ajili tu ya kujipatia kile
kinachoonekana kuwa ni “matokeo” ya haraka. Mengi ya mafundisho hayo ya kisasa
yanasukumwa na mawazo ya “mafanikio” yakikusudia kutafuta kitu fulani
“kinachofanya kazi” na hiyo ni “Mafanikio”. Hawa walimu wa kisasa wanaendelea
kubuni mawazo mapya pamoja na mitindo ya kufundisha. Hakuna hata mmoja
anayeweza kujihoji mwenyewe kuwa inakuwaje kila baada ya miaka michache
kunahitajika “mitindo” mipya, katika mtazamo wa Kitheolojia – hii ni upepo mpya
wa imani! Wala hakuna hata mmoja anayeweza kuuliza, kulitokea nini na ule upepo
wa imani uliopita? Au kutambua kwamba kanisa halihitaji mtindo mpya katika
mafundisho yake ya Imani isipokuwa ni marejeo kwa yale ambayo tayari
yamefunuliwa vizuri katika maandiko. Ikiwa tutakuwa waaminifu, tutapaswa kuungama
kwamba, mafundisho hayo mengi ambayo yanaendeshwa na wazo la mafanikio ni
matokeo yanayotujia moja kwa moja kutoka kwenye mila za kibiashara za Marekani
(U.S.A); mahala ambako kila kitu kinategemea malengo, matokeo pamoja na
mafanikio. Na Wakristo zaidi sana huko Marekani wameazima akili hizo au
wamechukua mtazamo na silka kutoka kwa ulimwengu na wameuingiza kanisani,
umewapelekea kwenye ubunifu wa mafundisho na matendo ya kutatanisha.( Bila
shaka, mimi sisemi kwamba, wazo la roho za kimaeneo linakuja kutoka kwenye
desturi za kibiashara, lakini huu msukumo kwa ajili ya mafanikio – ambao
umewapelekea Wakristo hawa kutumbukia katika ubunifu na udanganyifu).
Mwandishi na
mwalimu ambaye ni mmoja wa waenezaji wakuu wa mafundisho haya anaelezea juu ya
jambo ambalo nimeligusia hapo juu, kuhusiana na kukosekana kwa maandiko
yanayounga mkono mafundisho haya. Katika utangulizi wa kitabu chake
alichokiandika yeye mwenyewe kiitwacho “Territorial Spirits” (“Roho za
Kimaeneo”; Sovereign World Ltd. Ó1991 C.P.Wagner), amesema kuwa, amewahi
kutazama kwenye vitabu 100 huko kwenye seminari ya theolojia ambavyo
vimezungumzia kuhusiana na somo la malaika na mapepo, ili aweze kugundua
mafundisho yahusuyo roho za kimaeneo. Anaendelea kueleza kuwa, siku za leo ipo
haja kubwa sana ya kufanya utafiti kwa ajili ya somo hilo. Lakini kwa nini
tufanye utafiti? Je utafiti wa kwenye Biblia hautoshi? Je hatuna Biblia? Neno
la Mungu halitoshi kutuelekeza kuhusiana na jambo kama hili la msingi? Kwa
dhahiri kabisa sivyo hivyo, kwa kuwa yeye hawaaliki watu wafanye utafiti katika
Biblia. Ijapokuwa kwa hakika anajaribu kutafuta ushahidi kwa ajili ya
mafundisho hayo kwenye maandiko, kama tutakavyoweza kuona hapo baadaye, yeye
anaenda sehemu nyingine ili kuona iwapo anaweza kupata uthibitisho kwa ajili ya
ubunifu huu wa kigeni. Lakini anatuambia kwamba ni vitabu vitano tu kati ya 100
vilivyotaja kuhusiana na somo hilo la roho za kimaeneo, na kati ya hivyo vitabu
vitano, ni vitatu tu ambavyo angalau vinasema chochote kinachoweza kusaidia.
Lakini hakuna chochote kati ya vitabu hivyo ambacho kilistahili kujumuishwa
katika kitabu chake. Hii haishangazi kwa vile mafundisho hayo hayamo pia katika
Biblia – na mpaka sasa hakuna hata mmoja ambaye amebuni au kuyatumia kwa jinsi
hiyo, kwa kadri nifahamuvyo. Kwa hiyo, katika kitabu chake hicho anajumuisha
michango kutoka hasa kwa waandishi wa siku za leo ambao wanaoeneza mawazo ya
jinsi hiyo. Wagner alikuwa anafanya utafiti juu ya kanuni za ukuaji wa kanisa
na maombi, alipowafikia viongozi wa kanisa fulani ambao walikuwa wakifanya aina
hii ya maombezi dhidi ya roho za kimaeneo. Hapo, ilimpelekea kuingia ndani
zaidi ya mafunzo yake juu ya somo hili. Kama tulivyokwisha kuona katika makala
nyingine iliyopita, watu hao wanapofanya utafiti wao hawaanzi kwa kusoma Biblia,
isipokuwa wao huanza kwa kutegemea uzoefu wao wenyewe na “mafunuo ya kiroho”
wanayoyapokea. Ndipo hutafuta maandiko ambayo huyalazimisha au kuyafanya yaunge
mkono “mafunuo” waliyopokea. Nasi tutatazama maandiko hayo hapo baadaye. Lakini
napaswa kusema kuwa, hata hao viongozi wa makanisa – ambao waliiamini imani
hiyo ya kigeni, hawakubaliani wao kwa wao kuhusiana na mafundisho haya, na
namna ambayo yanapaswa kutumiwa. Kwa vile hayaungwi mkono na maandiko ya Neno
la Mungu, basi haishangazi kuona kwamba mmoja wa waenezaji wa mawazo haya
ameamua kusema kwamba kwa kuwa Mungu ni mwenye enzi, basi anafunua mbinu mpya
na bora kwa ajili ya uInjilisti wa ulimwengu mzima. Wanachomaanisha ni kwamba
Mungu anaufunua kwao ufunuo huu usiopatikana katika Biblia, na hivyo wanajihesabia
wenyewe mamlaka ya kitume! Yote hii inaonyesha jinsi wanavyoiacha imani, kwa
vile wanayainua mafununuo yao na uzoefu wao juu ya neno la Mungu.
Hebu sasa
tuyatazame kwa karibu yale yanayofundishwa na waandishi hawa wa kisasa kuhusu
vita vya kiroho.
Mafundisho
yao juu ya Vita vya Kiroho.
Wanaigawa
vita ya kiroho katika ngazi tatu. Kwanza, kuna kile wakiitacho mapambano ya
“ngazi ya chini”, ambayo wanamaanisha kutumia mamlaka ambayo Mungu amelipatia
kanisa lake kuwatoa mapepo toka kwa mtu mmoja mmoja. Hii imetolewa mfano wake
vizuri katika Injili na Matendo ya Mitume na hivyo siyo jambo lenye kuleta hoja
kwetu. Aina ya pili inaitwa mapambano ya “ngazi ya kishirikina” ambavyo
wanamaanisha kuwa ni kukabiliana na kuzifunga roho za uchawi, dini ya kishetani,
ibada za sanamu, na kadhalika, mambo ambayo kwa kawaida yanaleta athari zake
ovu kupitia kwa mtu fulani binafsi. Ngazi ya “juu” ya mapambano ya kiroho
inaitwa mapambano ya “kimkakati” au ya “kwenye anga za juu” ambapo maombezi
yanahitajika ili kuzitambua na kuzifunga roho mbaya za ngazi za juu, au mamlaka
na nguvu, ambazo zinatawala katika maeneo makubwa ya kijografia.
Hizi ngazi
mbili za mwisho ni mambo ya kukisia na ubunifu wa hawa waandishi wa kisasa,
kama tutakavyoweza kuona. Ile ngazi ya pili haina umaarufu mkubwa na
inaingiliana kwa kiasi fulani na ile ya tatu. Kwa hiyo nitazungumza kidogo juu
ya ngazi hii ya pili, tutakapoangalia vifungu vinavyohusiana nayo. Lakini ni
ngazi ile ya tatu ambayo mafundisho yao yanakazia, kwa hiyo kwa upana zaidi
tutakuwa tunatazama ngazi ya mwisho, kwa vile ndiyo hasa inayowakilisha
udanganyifu na hatari kubwa.
Ni namna
gani roho hizi mbaya zinatambulikana na watu kukabiliana nazo? Sawa, kwa wale
ambao wanaamini kuwa wameitwa ili kuhusika na aina hii ya vita, wanatumia muda
wao mwingi katika maombi kutafuta kutambua kwa njia za karama za kiroho na
“upambanuzi”, jina au aina ya roho (moja au zaidi ya moja) iliyoshikilia eneo
fulani – inaweza ikawa ni roho ya kiburi, uchoyo, tamaa mbaya au uchafu, ndipo
tena wanakabiliana nayo katika vita vya maombi na kuzifunga nguvu zake – hii
inaweza ikachukua siku kadhaa au wiki kadhaa. Ili kutambua ni roho gani
inatawala juu ya mji, wanafundisha pia haja ya kile wanachokiita kuwa ni
“kutengeneza ramani za kiroho”, kazi ambayo inahusisha uchunguzi wa historia ya
mji – hali ya mji huo kidini, kijamii na kikabila, na historia ya nyuma, hali
kadhalika kuhusu matendo maovu yaliyofanywa katika mji huo, au kufanywa na mji
huo, au yaliyofanywa dhidi ya mji huo – kurudi nyuma miaka zaidi ya mia au kama
si elfu na zaidi! Inafundishwa kwamba tendo hili litatusaidia sana kuzitambua
ni roho chafu za jinsi gani zinazoshikilia mji kwa nguvu sana ili kwamba tuweze
kuomba kwa ufanisi dhidi yake na kisha kuzifunga nguvu zake! Nilishughulikia juu
ya hoja hii ya kiushirikina katika ile makala yangu ya kwanza.
Baadhi ya
hawa wahubiri wa kisasa wanasema kwamba hawataweza kuhubiri Injili katika eneo
lolote lile hadi kwanza wawe wametambua roho mbaya zinazotawala na wakazifunga
nguvu zake. Lakini sasa Yesu hakutumia mtindo huu katika mji wowote aliouendea.
Hatusomi chochote kuhusiana na mtume Petro au Paulo akishiriki katika aina hii
ya “vita vya kiroho” kabla hajautembelea mji wowote ule; au kuhubiri Injili
hapo. Hatusomi chochote kile kuhusiana na mtume Paulo kuzifunga roho za uzinzi,
uchoyo au tamaa mbaya kule kwenye miji ya Efeso au Korintho kabla hajaanza kazi
yenye nguvu hapo. Wala hatusomi popote kwamba katika nyaraka zao kuwa mitume
hao waliwasihi watakatifu kuomba dhidi ya roho za kimaeneo, kama hawa waandishi
na wahubiri wa kisasa wanavyotutaka sisi tufanye!
Makosa
Mawili ya Kimsingi
Fundisho
hilo siyo tu kwamba ni nyongeza kwa Maandiko, bali kwa kweli linaielezea vibaya
na kuidhoofisha kazi yote ya Kristo pale Kalvari na jinsi Injili ilivyo. Na
tutaanza kwa kuyatazama makosa mawili ya kimsingi ambayo mafundisho hayo
yanawatumbukiza watu ndani yake.
Kwanza,
fundisho hili linakanusha au kupunguza ushindi mkamilifu ambao Yesu aliutimiza
pale msalabani. Mafundisho yenyewe hauyakiri kikweli ushindi halisi ambao
Kristo ameupata dhidi ya nguvu zote katika ulimwengu wa roho, kwa niaba ya
kanisa lake, kadhalika na kwa ajili ya wanadamu, wala hawa walimu hawaheshimu
kikweli na kujali mamlaka zote na haki ambazo Mungu anazo za kuwaelekezea watu
wake na kujenga kanisa lake.
Kabla ya
pale Kalvari, Yesu mwenyewe alikuwa akitembea huko na huko akihubiri habari
njema ya ufalme wa Mungu. Hali kadhalika aliwatuma mitume pamoja na wanafunzi
kuhubiri Injili ya ufalme wa Mungu na kuwatoa watu mapepo na kuwaponya wagonjwa.
Akiwa amepokea msamaha na ushindi juu ya majeshi ya uovu pale msalabani, Kristo
aliita, akatuma na akawatumia mitume vile vile na watu wengine katika kulijenga
kanisa lake. Tunajua kuwa watu wengi waliokolewa kupitia mahubiri ya mtume
Petro. Filipo alitumwa na Mungu kuwageuza wengi watokane na dhambi na uchawi.
Matendo 8. Na katika ile Matendo 11:19-21, tunasoma kuwa, “… mkono wa Bwana
ukawa pamoja nao, wao … waliohubiri Yesu ni Bwana kwa mataifa na watu wengi
wakaongezeka upande wa Bwana”. Mtume Paulo aliitwa na Mungu, Matendo 26:13-18;
katika ile Matendo 13:2 mtume Paulo alitumwa na Mungu. Watu hawa wote
walihubiri neno la Mungu kwa watu wengine, wakikiri kile ambacho Kristo
amekifanya pale Kalvari na watu wengi walimgeukia Bwana. Mitume waliwakomboa
waume kwa wake pia kutokana na roho za uovu na waliyakemea mapepo yaliyokuwa
yakitenda kazi ndani ya mtu mmoja mmoja. Matendo 13:8-11; 16:18; 19:12. Hayo
yote yalitokea pasipo hata kupata mafundisho yahusuyo na pasipo matumizi ya
mtindo huu wa kisasa ambao unaitwa “mapambano ya kimkakati”
Hebu niseme
hapa kwamba inapaswa iwe wazi kwetu, kwamba sio mahubiri yoyote na kila
mahubiri huwa na ufanisi. Mtume Paulo alikuwa makini katika kumhubiri Kristo,
lakini yeye alijikabidhi mwenyewe kwa ndugu zake pamoja na kwa kanisa, naye
alikuwa tayari kurejea nyumbani kwake katika mji wa Tarso, Matendo 9:26-31.
Baadaye tunamkuta kama mmoja wa manabii na walimu huko Antiokia, Matendo 13:1.
Paulo hakuhubiri tu mahali popote pale kulingana na mipango yake na ubunifu wake,
bali akiwa na ushirika na Mungu na akimtii Roho na kanisa, Paulo aliitwa na
Mungu kuihubiri Injili, Matendo 13:1, na alielekezwa na Roho maeneo ya kwenda
na maeneo ya kutokwenda, Matendo 16:6 – 10. Hivyo mtume Paulo anasema katika
Warumi 10:14 – 15. “…basi wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikiaje pasipo
mhubiri? Tena wahubirije wasipopelekwa?” Mtume Paulo pamoja na wenzake walikuwa
makini sana kuhusiana na wito huu wa kimungu – 1 Kor. 9:16,17 na alikuwa makini
zaidi pia kuwa angeweza kufanya kazi vizuri tu kulingana na wito wake, 2 Kor.
10:13-18.
Ikiwa
tutaenda mbali na wito wa Kimungu na karama; ikiwa tutaenda mbali na muda wa
Kimungu katika maisha yetu; ikiwa tutaenda mbali na Neno la Mungu – basi
tusitegemee kupata matunda ambayo Mungu anayategemea kutoka kwetu. Tunapaswa
kuwa watumishi wa Mungu, hii ina maana kwamba tunatakiwa kufanya yale tu
anayoyasema na kujikabidhi kwenye maelekezo yake na muda wake katika maisha
yetu. Hatutakiwi pia kwenda mbali zaidi ya karama na wito wetu. Hii inaweza
kuwa pengine ndiyo sababu wengine wanaenda pasipo kupelekwa? Inaweza kuwa ndiyo
sababu kwamba wanapata mafanikio kidogo au hawaoni mafanikio kabisa kutokana na
mahubiri yao. Juhudi ya jinsi hii ya wahubiri wasio na subira wanatafuta sasa
kutunga au kubuni mtindo fulani au mbinu ambazo zitaifanya kazi yao iweze
kufanya kazi vizuri na kuleta “mafanikio”! Inaweza ikawa ndiyo sababu wanaenda
mbali zaidi ya yale ambayo yanafundishwa na Maandiko ili kwamba wapate haya?
Ninafikiri kuwa mambo hayo pia yanachangia katika jambo hili lote la UInjilisti
wenye mafanikio pamoja na kushughulikia “mbinu mpya”. Hii yote haimaanishi kuwa
ikiwa tumetumwa na Mungu, basi siku zote tutaona ‘matokeo makubwa’, bali ikiwa
tuna shauku ya kumtumikia Mungu na kumzalia matunda na kiukweli kupeleka Neno
lake kwa watu, basi tutaenenda kwa kufuata Neno lake na Roho wake.
Kama
tusomavyo Injili na Matendo ya Mitume, tunaona kwamba watu wa Mungu walihubiri
na kushuhudia juu ya kifo chake na ufufuo katika utii wa amri zake na maongozi
yake au kwa kadiri fursa zilipojitokeza. Ijapokuwa walifahamu kuwa Kristo
ameangamiza mamlaka na uwezo, haina maana yoyote, kama tusomavyo katika habari
zao, kwa watu wa Mungu kuchukua UInjilisti “katika mikono yao wenyewe” na
kujaribu kuifanya kazi ya Mungu kwa ajili yake. Mitume hawakufanya mambo kwa
kukisia pale walipokuwa wakilitumia neno la Bwana au walipotumia uwezo na
mamlaka ambazo aliwapatia. Walimtii Mungu na Mungu aliwarejesha wengi kwake na
akadhihirisha nguvu zake kuu. Na Mungu aliupata utukufu! Hayo yote yalitendeka
pasipo hata kuzitambua au kuzifunga roho za kimaeneo! Hawakujaribu kuongezea
chochote kile juu ya yale ambayo Mungu alisema na kuyafanya ili kuufanya
uInjilisti uwe wenye mafanikio zaidi! Lakini hawa walimu wa kisasa pamoja na
wahubiri wanathubutu kuonyesha kwa mafundisho yao, kwamba yale ambayo Kristo
aliyafanya pale msalabani hayakutosha. Ndiyo, wanatangaza kwamba Kristo alipata
ushindi pale msalabani, lakini inaonekana kana kwamba hakuzivunja mamlaka na
enzi vya kutosha kwa ajili yao, kwa sababu wahubiri hawa wanaamini kuwa roho
chafu bado zina haki kisheria kuwashikilia watu katika giza na kifungo na kuwa
Injili haiwezi kupenya katika eneo linalotawaliwa na roho hizo. Wanafundisha
kuwa mtu anahitajika kwanza kufanya “vita vya kiroho” ana kwa ana na mamlaka
hizo pamoja na nguvu hizo kwa maombi, hadi kuzishinda nguvu zake kupitia maombi
kwanza, kabla Mungu hajazirejesha roho za watu kwake! Mawazo ya aina hii kwa
hakika ni ya jamii ya kiushirika tu na yenye milki ya ulozi zaidi kuliko kuwa
na mawazo ya kimaandiko. Mtazamo huu juu ya aina hii ya roho ya kimaeneo pamoja
na uwezo wao pamoja na aina hii ya kuzingatia katika maombi dhidi ya roho ya
uovu, hayapatikani katika maandiko ya neno la Mungu. Mtazamo huu unaweza
kumtukuza ibilisi kwa namna itakayowanyima watu wa Mungu ufahamu wa kweli na
nguvu ya Kristo ndani ya watakatifu wake na kupitia kanisa lake. Inawafanya
watu wamfikirie shetani zaidi badala ya kuweka mawazo yao kwa Kristo, na kwa
jinsi hiyo wanampatia shetani uwezo zaidi na utukufu na kuwanyang’anya
watakatifu ile imani yao ya kweli katika Mungu. Maandiko yanasema kwamba,
“Ijapokuwa hatujayaona mambo yote yakitiishwa chini ya nyayo zake, lakini
tunamwona Kristo.” Amina! Lakini sasa, badala yake walimu hawa wa kisasa
wanatutaka sisi tuyaone mapepo! Ni mafundisho madhaifu na manyonge kama vile
yenyewe yalivyo si ya kibiblia. Na hao walioyahamasisha mafundisho hayo ndio
huwa wa kwanza kukubali katika vitabu vyao kwamba watu wameharibiwa walipokuwa
wanajaribu kutumia mbinu hizo. Mafundisho hayo ni kashfa dhidi ya mamlaka ya
Mungu na shambulizi dhidi ya ushindi kamili wa Kristo alioupata pale Kalvari,
ambao ndio unaomruhusu kulijenga kanisa lake kulingana uradhi wa mapenzi yake
mwenyewe. Katika uweza ambao Mungu aliutumia katika kumfufua Kristo kutoka
katika wafu. (Efe 1: 19-23)!
Ndiyo
tunatambua kile kinachofundishwa na maandiko, kwamba mfalme wa uweza wa anga ni
ile roho itendayo kazi sasa katika wana wa uasi; Efe 2:2. Shetani
huzungukazunguka kama simba angurumaye akiwafunga wengi kuyatenda mapenzi yake
na hafanyi lolote isipokuwa ni kuua, kunyang’anya na kuharibu. Yeye hudanganya
na kuwafunga wengi katika vifungo. Mambo hayo pamoja na mengineyo yanafundishwa
ndani ya maandiko, na wala hiyo sio hoja yetu tena hapa. Nami sisemi hapa
kwamba hatuwezi kuomba kwa Mungu, kuhusiana na mambo ya aina hii; wakati ambapo
tunajua hali na watu ambao wanahitaji neema ya Mungu, rehema pamoja na wokovu
wake. Lakini linapokuja jambo la uenezi wa Injili na jinsi inavyoenezwa na
kubadilisha maisha ya watu, ndipo tunaweza kusema kuwa mafundisho hayo ya
kisasa yameenda nje ya maandiko, na yametumbukia katika kasoro na udanganyifu –
yanawafanya watu wawe shabaha ya roho za udanganyifu. Wanakubali kuwa Kristo
amepata ushindi pale kalvari dhidi ya shetani, lakini bado wanaamini kwamba
wanatakiwa pia wapate ushindi zaidi juu ya roho zinazotawala ju ya maeneo yote
yanayokaliwa na watu.
Ni nini
kinaipatia roho hizo za kimaeneo haki ya kisheria kukamata mamlaka za aina hii
juu ya watu, kiasi kwamba hata iifanye Injili isiwe yenye mafanikio katikati
yao? Haya ati wanasema ni zile dhambi zilizopita za jumuia hiyo au mkoa na ile
laana iliyowekwa juu yake kwa sababu ya dhambi hizo! Napenda niwaambie ukweli,
wanachokifanya hawa walimu wa kisasa ni kuzijaza akili za watu wa Mungu mambo
yasiyo ya kiInjili yenye ushirikina mtupu na yenye kasoro nyingi. Kristo
amezichukua dhambi za ulimwengu mzima na amelipia gharama kubwa isiyohesabika
ili kufanya hayo. Kristo ni mwenye mamlaka zote za juu – ni Mkuu. Shetani
anaweza tu akaenda pale ambapo Mungu amemruhusu kwenda. Sawa, maandiko yanakiri
kuwa ipo haja ya maombi, kuhubiri, uInjilisti, kazi pamoja na ukombozi wa mtu
mmoja mmoja kutokana na mapepo; lakini kadiri ya haja ya kuihubiri Injili
inavyohusika, bado maandiko hayakiri kwamba kuna haja ya toleo lingine zaidi ya
lile alilolinunua tayari Kristo pale msalabani kwa ajili ya ulimwengu wala
maandiko hayakiri kwamba “dhambi zile za kihistoria” zilizopita za maeneo ndizo
zinaipatia roho za kimaeneo haki ya kisheria kuzuia Injili; wala pia maandiko
hayakiri kuwa ipo haja ya watakatifu kujiingiza moja kwa moja katika
makubaliano ya kiroho na hizo roho za kimaeneo kana kwamba roho hizo
zinahitajika kufungwa kabla ya Injili kufanyika na kuenezwa kwa mafanikio
yanayopaswa ( tafadhali angalia makala yangu ya kwanza ambamo jambo hili
limeelezwa kwa undani zaidi ).
Wakati mtume
Paulo alipokuwa Athene, hawakupatikana watu wengi waliomgeukia Mungu lakini
pamoja na hali hiyo, si Paulo mwenyewe wala si maandiko ya Neno la Mungu
yanapohesabu hali hiyo ya watu kutoipokea Injili kuwa ilisababishwa na nguvu
kuu na mamlaka au haki ya roho za uovu kupinga Injili au kazi ya Mungu. Mtume
Paulo hakuianza kuzishughulikia roho za kimaeneo katika maombi kwa sababu ya
kuonyesha “upungufu wa mafanikio” katika huduma yake. Mtume Paulo alikuwa na
ufahamu mkubwa zaidi na mafunuo kuliko hawa walimu wa kisasa, lakini yeye
hakukimbilia kwenye “mbinu za kiwango cha kimkakati” ili kuzishinda “roho ya
kuabudu sanamu” ambazo zilidhaniwa “kutawala” katika mji wa Athene, katika
jitihada yake ya kuushinda upungufu huu wa mwitikio katikati ya watu. Unaona,
hawa walimu wa kisasa wao wanasema kwamba, watu kwa kweli hawapo huru kuitikia
Injili hadi hapo tutakapokuwa tumezifunga roho za kimaeneo! Mmoja wa waandishi,
kwa kweli anapendekeza kuwa roho za kimaeneo zinazotawala kule Athene, zilikuwa
zenye uwezo mkubwa kiasi kwamba zilimfanya mtume Paulo kuzishindwa na eti hiyo
ndiyo sababu alipata mafanikio kidogo sana huko! Lakini sio Paulo wala maandiko
ya neno la Mungu yanayohitimisha jambo hilo kuhusu aina hii ya “upungufu wa
mafanikio”. Badala yake, mtume Paulo yeye anaendelea mbele na safari yake kwa
mapenzi yake Mungu na mpaka anapoingia katika mji wa Korintho, hatuoni popote
pale panapomuonyesha akijishughulisha na kazi ya kuzifunga roho za kimaeneo, na
bado watu wengi sana walimgeukia Bwana. Maandiko hayaelezei sababu hasa
inayofanya watu wengi zaidi wamgeukie Bwana katika eneo moja kuliko jingine,
lakini yanatupa vidokezo na kutuelekeza kwenye kanuni fulani fulani, ambazo
tutaziangalia hivi punde.
Lakini jambo
moja lenye uwazi ni kwamba maandiko hawayahesabii “mafaniko” au “kupungua kwa
mafanikio” kwamba imetokana na mtu mmoja ambaye ameweza kuzishinda roho za
kimaeneo zinazotawala au la.
Ninadhani
kuwa kama hawa walimu wa kisasa wangekuwepo kule nyakati zile za Paulo
alipotembelea Athene, wangeweza kushauri kuwa Paulo aweze kuhudhuria masomo
katika moja ya seminari ya Kithiolojia ili aweze kujifunza kwanza “kanuni za
kukua kwa kanisa”. Pengine wangeweza kumwelezea pia kuwa mtindo wake anaoutumia
katika UInjilisti bila shaka “haufanyi kazi” vizuri na hivyo anapaswa kuzisomea
“mbinu mpya za mafanikio” ya uenezaji wa Injili, ambazo ndizo zimethibitishwa
kuleta mafanikio! Wangeweza kumwambia kuwa yote aliyoyafanya amekosea kwa
sababu tatizo halikuwa ni Wathene binafsi isipokuwa ni ile roho ya kieneo ya
kuabudu sanamu ndiyo iliyokuwa inawazuia watu kule wasiweze kuiitikia Injili.
Mtume Paulo angelazimika kufundishwa vita vya kiroho iwapo angependa kuona
mafanikio katika kuieneza Injili! Angepaswa kujifunza kuhusu kutambua majina ya
roho chafu za kimaeneo na namna ya kuzikabili katika kuzifunga kwa maombi!
Asingetazamia kupata mafanikio hadi kwanza afahamu jinsi ya kuyafanya mambo
haya! Lakini sasa hebu fikiria jinsi Paulo alivyoweza kuwashughulikia walimu wa
uongo walionyemelea makanisa ya Galatia; sifikirii kwamba angeweza kuvutiwa kwa
vyovyote vile, badala yake angeweza kuwakemea kwa nguvu kwa ajili ya kuichafua
Injili ya Kristo.
Hii ndiyo
sababu inayonifanya niseme kwamba, mafundisho hayo wanayotuletea ni kashfa
dhidi ya mamlaka na busara za Mungu, ambaye huwaita na kuwatuma watu kwenda
kuhubiri Injili kulingana na amri na mafundisho ambayo ameyaweka kwa ajili
yetu. Hawa waandishi wa kisasa wanaweka busara yake Mungu na mamlaka za utawala
wake katika maswali. Wangeweza kuiita huduma ya Paulo kwa ajili ya watu wa
Athene ni jambo “lililoshindwa”. Wako makini kutafuta mafanikio kiasi kwamba
wanadiriki kuisukumilia mbali amri ya Kristo – ya kwenda ulimwenguni kote
kuihubiri Injili – sasa kinyume chake wao wanazunguka huku na huko wakianzisha
amri zao wenyewe, na hivyo wanajiweka kinyume na busara za mamlaka ya Mungu na
utawala wake juu ya mambo haya.
Hata kama
Mungu alibariki au kama aliwaruhusu waweze kujaribiwa, hata kama kulikuwa na
mwitikio mkubwa wa watu au kidogo – bado mitume wa mwanzoni kabisa, wao pamoja
na kanisa waliendelea kumwangalia Mungu; wakijikabidhi kwake, wakimwamini yeye
na kumtukuza yeye! Hivyo ndivyo walivyofanya! Na kama hapakuwepo na mwitikio
sana, hawakumtilia shaka Mungu na kuanza kukimbia huko na kuko kujifunza na kubuni
“kanuni mpya za ukuaji wa kanisa”! Wao walikuwa wakiomba na wakihubiri na
walikuwa imara katika imani na upendo; kama vile tusomavyo katika kitabu cha
Matendo ya Mitume, lakini wao pia hawakujishughulisha katika aina ya maombi
yanayohusika na kuzishambulia roho za kimaeneo kama ambavyo inavyohamasishwa na
waandishi hawa wapya.
Ijapokuwa
wanakiri juu ya ushindi wa Kristo pale Kalvari, lakini mafundisho yao hayo
yanaufanya wokovu wa roho za watu uonekane kuwa unategemea matokeo ya aina
fulani ya mapambano ya ana kwa ana kati ya majeshi ya kiroho ikiwepo roho chafu
kwa upande mmoja, ikipambana na karama za Roho na maombezi ya Wakristo kwa
upande mwingine; vita hiyo inayoelezwa humo ni ubunifu wa akili zao wenyewe tu
( ambayo wanaiazima kutoka kwenye milki za ulozi. Vitabu vya ubunifu – kama
vile kitabu cha Frank Perret ) na vinajaribu kuongezea kitu kingine juu ya
ushindi ambao Kristo aliupata pale Kalvari (msalabani). Katika maandishi yao,
wakati mwingine inatolewa mfano wa nguvu za upinzani zilizo sawa sawa
zikipigana dhidi ya roho. Wanaonyesha kuwa iwapo hutazishinda roho za kimaeneo
zilizo za kienyeji na za kimaeneo zinazomiliki eneo fulani, basi kazi ya Injili
na wokovu wa nafsi haiwezi kufanikiwa ipasavyo. Katika kutimiza hamu yao ya
kupata “mitindo ya mafanikio”, wahubiri hawa pamoja na waandishi wao
hawajikabidhi katika Neno la Mungu na maelekezo yake ambayo Yesu ameyakamilisha
pale msalabani – wanafanya hayo yote kwa ajili tu ya kutafuta matokeo. Nasema
tena kwamba mawazo hayo ni ya kuanzishwa toka duniani, hayamtukuzi Mungu,
badala yake yanatukuza mafundisho yasiyothibitishwa ambayo husababisha
machafuko na kukata tamaa, na zaidi ya yote yanamtukuza shetani.
Mafundisho
yasiyothibitishwa ambayo husababisha kuchanganyikiwa na kukata tamaa.
Lakini hebu
niseme hapa kuwa shauri lao halijathibitishwa! Bila shaka haionyeshi kwamba
wanaweza kwa kweli kuonyesha kuwa jamii imebadilishwa kutokana na mafundisho
hayo yao. Zaidi ya hayo yote, wengi wa mashabiki wa mafundisho hayo wanaishi
Marekani (USA). Je huko kwao yameleta mabadiliko gani? Mchungaji mmoja wa
kanisa moja kubwa kule New York aliwahi kuandika kitabu kuhusu kazi za kanisa
lake na jinsi Mungu alivyopambana na mafundisho haya ya kisasa – na jinsi hata
yeye alivyoumizwa katika moyo wake kuona jinsi ambavyo dhana hii isiyo ya
kibiblia inavyoweza kushikilia akili za watu wa Mungu na inaendelezwa
kufundishwa nchi nzima. Lakini analiweka swali lile lile na linalofanana –
kuelezea ni kwa nini basi, iwapo mafundisho hayo ni ya ukweli, mbona
hayabadilishi miji ya Amerika – tunaambiwa na watu wengine kuwa California ya
kusini ni mji unaowakilisha kituo cha vivutio vya matamanio katika ulimwengu.
Yako wapi basi mabadiliko hayo makubwa katika miji ya Marekani iwapo mafundisho
hayo ni ya ukweli? Lakini mtu mwingine anaweza kuuliza hivyo hivyo kuhusu miji
mingine mingi pamoja na nchi. Mafundisho hayo hayo yamekuwa yakiendeshwa
Uingereza karibu miaka 15 sasa kwa kadiri ninavyofahamu, lakini sasa, yako wapi
– basi mabadiliko hayo makubwa yaliyoahidiwa na mafundisho hayo? Ninafikiri
kuwa watu wengi wangekubali kwamba, sio jamii tu yenye hali mbaya, isipokuwa
kanisa leo limo katika hali mbaya zaidi; kwa kusema kwa ujumla, liko katika
hali mbaya kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita. Tendo mojawapo lililosababisha
machafuko, matengano, maumivu ya mioyo, kuchanika kwa makanisa, kadhalika na
kugawanyika kwa makanisa, je huko ndiko kuzaa kwa wingi kwa imani hiyo mpya!
Mashabiki wa
mafundisho hayo wametengeneza mkanda wa video, ili kuwashawishi watu waone
namna ambavyo vita hivyo vya kiroho vinavyoleta mafanikio. Baadhi ya watu
wengine ambao wamechunguza yale yanayodaiwa na mikanda hiyo ya video, kwa
kuzuru hadi kwenye maeneo hayo waliyo chukulia mkanda huo pamoja na kupata
habari sahihi za maeneo hayo, wanatuambia kuwa mambo mengi, yaliyodaiwa ndani
ya mikanda hiyo yametiwa chumvi – na mara nyingi ni habari za uongo. Wale
wanaoamini katika imani au mafundisho hayo, kwa uasili wa kutosha wanaamini
kwamba “inafanya kazi” na wanajaribu kuonyesha watu kuwa ni kutokana na mtindo
wao mpya wa kuomba dhidi ya roho za kimaeneo, ndiyo iliyoleta mafanikio makuu
pale Injili ilipobanwa katika jumuiya fulani fulani. Lakini hatuoni kuungwa
mkono na maandiko ya Neno la Mungu katika maeneo hayo; na wala haiwezi
ikaonyeshwa kuwa hilo limekuwa ndiyo “ufunguo” au “jawabu” la ufanisi wa
uInjilisti kwa namna ya kimatendo, mbali ya malalamiko ya hadithi zao.
Kwa kweli
kitabu kimeandikwa ambacho nimekitaja hapo punde tu, kwa usahihi kabisa ni kwa
sababu kumekuwepo na machafuko pamoja na maumivu ya moyo yaliyosababishwa na
mafundisho hayo. Mwandishi wa kitabu hicho yeye mwenyewe pia anaamini katika
vita vya kiroho dhidi ya roho, lakini anatueleza kuhusiana na kukata tamaa
pamoja na hofu iliyowanyemelea wakristo waliokuwa na matazamio ya hali ya juu
ya mafanikio kutokana na mafundisho hayo. Lakini hatimaye waligundua kuwa
haikufanya kazi yoyote; ile kama walivyotarajia na hata ikawasababishia
majanga! Hali hiyo imewasababishia kujisikia ni watu wawezao kunaswa na shida,
hofu na machafuko! Ingawaje anajaribu kuonyesha kuwa mambo yaliwaharibikia kwa
sababu ya ongezeko na ujinga wa watu wenyewe wa kutokujua kanuni za aina hii ya
mapambano; mbali ya hayo yote kitabu hicho pia kinakazia ukweli kwamba, upepo
huu mpya wa imani sio huo ambao mashabiki wake wamelalamikia kuwa ndio, na wala
hautoi matokeo kwa namna ambayo hawa waandishi wapya wangetupelekea sisi
tuamini hivyo.
0 Comments