Mwenyekiti
wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheir James, amesema wakati wa
kufanya kazi kwa woga ndani ya umoja huo umepitwa na wakati.
Akizungumza
na wanachama wa CCM na jumuiya zake visiwani Zanzibar, alisema huu ni wakati wa
kufanya kazi kwa ushirikiano badala ya kumuabudu mtu kutokana na cheo chake.
Alisema
kiongozi anayejitambua ni yule anayefanya kazi kwa maslahi ya vijana wenzake na
kilichobaki kwa sasa ni kupambana ili jumuiya hiyo ya vijana iweze kufika mbali
kwa maslahi ya vijana na taifa kwa ujumla.
Aidha,
alisema wakati wa vijana wanaopenda kulalamika umefika mwisho hivyo ni vyema
wakajitahidi kufanya kazi bila ya upendeleo na woga.
Aliwataka
viongozi wenzake katika jumuiya hiyo kuanza kuhakiki mali za chama na aliyekuwa
haendani na kasi ya chama hicho awapishe wanaoweza.
"Umegombania
nafasi na tumekupa, sasa tufanyeni kazi ili vijana wajue thamani ya
uongozi," alisema.
Kheir
alisema uhakiki wa mali za chama hicho kwa upande wa Zanzibar utafanywa na
Wazanzibari wenyewe na atahakikisha anapatiwa ripoti ya uhakika kwenye taarifa
watakazozipeleka kwa uongozi wa juu na uhakiki wa watumishi hewa pia
utaangaliwa.
Makamo
Mwenyekiti wa Umoja huo, Tabia Maulid Mwita, alisema yupo tayari kufanya kazi
kwa ushirikiano wa hali ya juu na vijana wote na kuwashukuru kwa kumchagua
kushika nafasi hiyo na kuendeleza ahadi zake alizoziahidi kipindi cha kampeni.
Aidha,
aliwataka vijana kuacha makundi kwa kuwa uchaguzi umekwisha hivyo atahakikisha
haki inatendeka bila ya kumuonea mtu wala kujali cheo chake na kufanya maamuzi
kwa matakwa yake bila ya kumshauri mtu.
"Vijana
ndio jeuri ya chama ila kwa anayejitambua na sio kukaa kutukana katika majukwaa
kijana mzuri ni yule anayependa kusikiliza ushauri wa wakubwa wake,"
alisema.
Mapema
akitoa utambulisho kwa viongozi, Kaimu Katibu wa Umoja huo Zanzibar,
Abdulghafar Idirissa Juma, alisema Umoja huo utaangalia upya vitega uchumi
vyake ili viweze kuleta tija kwa wanachama na kuiendeleza jumuiya yao.
Akizungumzia
mradi wa Darajani alisema kuwa ulihodhiwa na baadhi ya viongozi wa serikali
hivyo alimtaka Mwenyekiti wa Umoja huo kulifuatilia suala hilo ili mipango
iendelee na mradi huo uweze kuleta tija kwa vijana na taifa kwa ujumla.
0 Comments