Serikali iko
katika mchakato wa maandalizi ya muswada wa sheria ambayo itasimamia sekta ya
nyumba, hivyo kuondoa changamoto ya wamiliki kudai kodi ya pango ya zaidi ya
mwezi mmoja.
Naibu Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema hayo bungeni
leo Ijumaa Novemba 17,2017 akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu
(CCM), Halima Bulembo.
Halima
katika swali lake amesema vijana ambao ni kati ya asilimia 56 na 60 nchini,
wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa ya kodi ambayo
hutakiwa kulipa kwa kipindi cha mwaka mmoja au miezi sita.
"Serikali
inasemaje kuhusu kuleta sheria itakayofuta tabia ya wenye nyumba kulazimisha
kulipwa kodi ya mwaka?" amehoji mbunge huyo.
Akijibu
swali hilo, Mabula amesema Serikali imeliona tatizo hilo na ipo katika mchakato
wa kuandaa muswada wa sheria utakaosimamia sekta hiyo.
Mabula
amesema baada ya kukamilika kwa sheria ambayo itaunda chombo cha kusimamia
sekta hiyo, wapangaji hawatalipa kodi ya mwaka wala miezi sita tena bali
watalipa kwa mwezi na kuweka amana ya miezi mitatu.
Katika swali
la msingi, Halima amesema kumekuwa na upandaji holela wa gharama za pango kwa
nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
"Je
Serikali haioni kuna haja ya kudhibiti upandaji holela ambao unaathiri wananchi
wengi kutokana na kipato chao?" amehoji.
Akijibu,
Mabula amesema utaratibu wa urekebishaji wa viwango vya kodi za shirika hilo
husimamiwa na bodi ya wakurugenzi ambayo imepewa mamlaka ya kisheria ya
kusimamia kodi ya pango na kuidhinisha viwango vya kodi vinavyotozwa kwa
wapangaji wa nyumba za shirika.
"Kwa
mara ya mwisho bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa iliidhinisha
viwango vipya vya kutoza kodi kwenye nyumba za shirika mwaka 2011 ambavyo
ndivyo vinavyotumika mpaka sasa," amesema.
0 Comments