Rais Dk John
Magufuli ameagiza Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam kuvunja sehemu ya jengo
la TANESCO na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo katika eneo la hifadhi ya
barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja la Ubungo.
Rais ametoa
agizo hilo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Ndyamukama Julius
wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo la Ubungo, baada ya kuejea jijini Dar es
Salaam, akitokea kijijini kwake Chato, mkoani Geita.
"Sheria
ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita tisini kila upande kutoka
katikati ya barabara hivyo ni lazima sheria hiyo iheshimiwe ili kuharakisha
ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu katika eneo hilo la Ubungo uanafanyika bila
vikwazo kwani sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali
yenyewe'' Taarifa ya Ikulu, imemkariri Rais Magufuli akisema.
Rais Magufuli
ameiagiza TANROADS kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa
kilomita kumi na sita (16) kutoka eneo linapoishia Daraja la ghorofa tatu
katika eneo la Ubungo kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisha
usafiri katika jiji la Dar es salaam.
Pia Rais
amewataka Wakandarasi wanaojenga Daraja la Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi
wa madaraja hayo usiku na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya
muda huo katika kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji la Dar es salaam.
''Dar es
salaam ni jiji la kibiashara hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri
iweze kurahisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje
ya jiji la Dar es salaam'' amesema Rais Magufuli.
Mhandisi wa
Masuala ya Usalama wa Ujenzi Mhandisi Richard Baruani amemueleza Rais Magufuli
kuwa Ujenzi wa Daraja la Tazara umefikia asilimia 64 ambapo Daraja hilo
linatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2018.
Kwa upande
wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo, Mhandisi Mshauri Reginald Kayanga amesema ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi Desemba
2017.
Katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dare es salaam,
Mhe. Rais amepokelewa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda na viongozi wengine wa mkoa.
Baada ya
kutoka Uwanja wa Ndege, Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu wa Rais
pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam,amekagua Ujenzi wa Daraja la juu Tazara
( Tazara Fly-Over) na Ujenzi wa Daraja la ghorofa tatu la Ubungo ( Ubungo
Interchange)
0 Comments