Wakazi wa
Kata ya Moita wameombwa kumchagua mgombea wa CCM ili wapate maendeleo na
kuachana na ahadi alizowapa, Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati kuu,
Chadema, Edward Lowassa.
Lowassa
aliyewahi kuwa mbunge wa Monduli ndiye aliyezindua kampeni za udiwani za
Chadema katika kata hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwaahidi wananchi kuwa
hatawasahau na ataendelea kushirikiana nao, kwani aliwaacha wakiwa tayari wana
umeme, maji na shule mbili za kata.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaban Mdoe akizungumza katika kampeni
eneo la Moita Bwawani, alisema wananchi wasidanganyike.
Mdoe alisema
kwamba wakimchagua mgombea wa CCM, Prosper Meyani kero zao zitapatiwa ufumbuzi,
ikiwamo kero ya maji na barabara.
“Msidanganywe
na Chadema, hawawezi kutatua kero zenu, alikuwepo diwani wao, hadi amejiuzulu,
mbunge wa zamani Lowassa hivi sasa hawezi tena kuwasaidia,” alisema.
Awali,
aliyekuwa diwani wa kata hiyo na kujiuzulu, Edward Sapunyo alisema aliamua
kujiuzulu baada ya kunyimwa ushirikiano na madiwani wa Chadema.
Alisema kila
mradi ambao alikuwa anaomba katika kata hiyo alinyimwa na hivyo akaona hana sababu
ya kubaki bali arejee CCM.
Kabla ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Sapunyo ambaye alikuwa mwenyekiti wa halmashauri
ya Monduli kupitia CCM, alisema chaguo sahihi katika kata hiyo ni mgombea wa
CCM.
Halmashauri
ya Monduli hadi sasa inaongozwa na Chadema kutokana na kuwa na madiwani 18 na
CCM madiwani tisa.
0 Comments