Katika matokeo yaliyokuwa yametangazwa kufikia saa tatu
asubuhi Jumatano, Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alikuwa akiongoza akiwa
na kura 7,461,933 (54.64%) akifuatwa na Raila Odinga wa muungano wa upinzani
National Super Alliance (Nasa) aliyekuwa na kura 6,079,136 (44.51%). Matokeo
hayo ni ya vituo 36659 kati ya 40,883.
Kura ambazo zilikuwa zimeharibika kufikia wakati huo ni
353,389.
Muungano wa Nasa umepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa
na tume hiyo na kusema si sahihi.
Bw Odinga amesema IEBC imefanya makosa kwa kutangaza matokeo
hayo bila kuwaonyesha maajenti wa vyama Fomu 34A, kubainisha matokeo hayo
yametoka katika vituo gani.
Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa
kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati
uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo.
Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili
asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.
Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza
uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia
kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo
vilivyochelewa kufunguliwa.
Mambo kumi yasiyofaa kukupita kuhusu uchaguzi mkuu Kenya
2017
Wengi wanahofia uwezekano wa kutokea tena kwa ghasia za
baada ya uchaguzi sawa na ilivyotokewa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Watu zaidi ya 1,100 walifariki na wengine 600,000 kuachwa
bila makao.
Tume ya uchaguzi imetangaza matokeo kutoka kwa vituo 36659
kati ya jumla ya vituo 40883 ambapo:
Uhuru Kenyatta wa Jubilee ana kura 7,461,933 (54.64%)
Raila Odinga wa ODM kura 6,079,136 (44.51%)
Joseph Nyagah (huru) 33,710 (0.25%)
Abduba Dida wa ARK 29,411 (0.22%)
Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance 23,976 (0.18%)
Japheth Kaluyu (huru) 10,316 (0.08%)
Cyrus Jirongo wa UDP 10,019 (0.07%)
Michael Wainaina (huru) 7,919 (0.06%)
Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 353,389
Ili kushinda, mgombea urais anahitajika kupata zaidi ya
asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na angalau asilimia 25 katika kaunti 24 kati
ya kaunti 47 nchini humo.
Iwapo hakuna mgombea atakayetimiza hilo, basi uchaguzi wa
marudio utafanyika katika kipindi cha siku 30.
Kujitokeza mapema
Wapiga kura walianza kujitokeza alfajiri na mapema kupiga
kura.
Foleni ndefu zilishuhudiwa katika vituo vingi, na kwingine
visa vya watu kuumia katika mkurupuko wa kupanga foleni vituo vilipofunguliwa
viliripotiwa.
Katika moja kati ya vituo vinne nchini humo, maafisa wa IEBC
walikuwa wamesema kwamba hakuna huduma nzuri ya mtandao maana kwamba wasimamizi
wa uchaguzi katika vituo hivyo watahitaji kusafiri hadi ameneo yenye huduma
nzuri ya simu kutuma matokeo kikamilifu.
Kumekuwa pia na taarifa kwmaba mwanamume mmoja ameuawa
katika makabiliano kati ya wafuasi wa wagombea wawili katika kaunti ya Kilifi,
pwani ya Kenya.
Lakini kulikuwa na kisa cha kutia moyo pale mwanamke mmoja
alipojifunzua mtoto msichana alipokuwa kwenye foleni akijiandaa kupiga kura
Pokot Magharibi.
Pauline Chemanang alisema kujifungua kwake ni baraka na
akampa mtoto wake jina Kura, kwa mujibu wa kituo kimoja cha redio.
Rais Kenyatta, baada ya kupiga kura yake kituo cha Mutomo
eneo lake la nyumbani la Gatundu, kaskazini mwa Nairobi, alisema kwamba yuko
tayari kukubali matokeo ya uchaguzi huo.
"Kwa wapinzani wangu, kama nilivyosema mara nyingi
awali, ikitokea kwamba washindwe, basi hebu tukubali uamuzi wa wananchi. Nina
nia, mwenyewe, kukubali nia ya wananchi," amesema.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipiga kura yake katika
mtaa wa Kibera, Nairobi.
Akiongea nje ya kituo hicho, aliwahimiza wafuasi wake:
"Hebu tujitokeze kwa wingi na tupige kura."
0 Comments