Na Mwandishi Wetu
Siah Malle ni mfano mzuri wa mwanamke ambaye amefanikiwa kuvunja
dhana iliyojengeka na kuwagawa wanawake na wanaume kwenye uwanja wa taaluma
mbalimbali duniani. Safari yake ya kuwa jaji katika Kongamano na Maonesho ya 8
ya Wanawake Wahandisi Tanzania (TAWECE) ni uthibitisho tosha kuwa ari na bidii
yake katika tasnia ya uhandisi imezidi kumuinua.
Alipokuwa anakua, Siah alivutiwa na ulimwengu wa sayansi na
teknolojia. Kaka yake ambaye ni mhandisi wa ujenzi, alichochea shauku yake
katika kuingia kwenye tasnia ya uhandisi na alidhamiria kufuata nyayo zake.
Lakini pia kwa kutiwa moyo na walimu wake, alisoma sayansi
na hisabati katika elimu ya sekondari na kufanikiwa kufaulu vizuri katika
masomo hayo.
Baadaye Siah aliendelea na elimu yake katika kozi ya
uhandisi ngazi ya stashahada ambayo alisoma kwa muda wa miaka mitatu katika
Chuo cha Ufundi Arusha.
Mmoja wa walimu wake aliyefahamika kwa jina la John Mbando,
alitambua uwezo wake mapema na kumtia moyo katika fani hiyo kisha kumshawishi
kuachana na uhandisi wa ujenzi na kubobea katika uhandisi wa mitambo.
Mbando alimshawishi kuwa uhandisi wa mitambo kuwa una
manufaa mengi, ikiwa ni pamoja na kuajiriwa, manufaa na kubuni vitu mbalimbali
ambavyo vinatatua changamoto au matatizo yanayoikumba jamii.
Hali hiyo ilisababisha mapenzi ya Siah katika uhandisi wa
mitambo kuongezeka na alidhamiria kuingia katika taaluma hii.
Baada ya kuhitimu vizuri stashahada yake, Siah alisoma kwa
miaka mitatu katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ambako alihitimu
Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Mitambo na kupata alama zenye wastani wa (GPA)
4.3 na kutunukiwa tuzo ya Mwanafunzi Bora wa Kike aliyehitimu mwaka wa kuhitimu
2019.
Mwalimu wa Siah, Mbando ndiye aliyefanikisha safari muhimu ya mwanadada huyu ambaye sasa ni mhandisi mbobevu.
Hakumfundisha tu ujuzi wa kiufundi wa uhandisi wa mitambo,
lakini pia alimjengea dhima nzima ya umuhimu wa kuzingatia maadili, mawasiliano
na kufanya kazi kwa pamoja.
Alimhimiza kufuata ndoto zake na kamwe asikate tamaa, hata anapokabiliwa na changamoto. Uzoefu wa Siah ni ushuhuda wa nguvu ya ushauri na athari ambayo mwanamke au mtu yeyote anaweza kuwa nayo kwenye kazi na maisha ya kila siku.
Baada ya kumaliza masomo yake, Siah aliajiriwa na kampuni ya
Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa ajili ya mafunzo ya ufundi mitambo kama
mhandisi wa mitambo.
Leo, anafanya kazi kama Mratibu 2 – katika idara ya
inayoundwa na timu ya wahandisi. Anafurahi kuwa sehemu ya kampuni hiyo
inayojitolea kuwajibika kwa kwa jamii kwa namna mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuwajengea uwezo zaidi wafanyakazi wake bila kujali jinsia huku ikiendelea na
shughuli za uchimbaji madini mkoani Geita.
Katika GGML, Siah amepata fursa ya kufanya kazi katika miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kubuni na kutekeleza ufumbuzi wa nishati endelevu.
0 Comments