
Mchezaji wa kiungo cha mbele wa Liverpool na timu ya taifa
ya Senegal Sadio Mane amekubali mkataba wa muda mrefu kuendelea kucheza
Anfield.
Mchezaji huyo mwenye miaka 26 alijiunga na klabu hiyo kutoka
Southampton kwa mkataba wa miaka 5 mnamo Juni 2016 kwa thamani ya £ milioni 34.
Tangu hapo amecheza mara 89 katika mashindano yote ya timu
hiyo ya Jurgen Klopp na kufanikiwa kufunga magoli 40.
"Ninafurahia sana kurefusha muda wangu Liverpool. Ni
siku nzuri mno kwangu na huu ni uamuzi bora kabisa katika kazi yangu,"
amesema.
Mazungumzo kuhusu mkataba huo unaodumu hadi 2023,
yaliidhinishwa mwishoni mwa msimu uliopita lakini yamekamilishwa hivi punde tu.
"Natazamia kila kitu - kuisaidia timu, kuisaidia klabu
kutimiza ndoto yetu hususan kushinda mataji," aliongeza.
"Daima nimekuwa nikisema, nilipojuwa nina nafasi kuja
hapa sikufikiria mara mbili. Klabu muafaka, kwa wakati muafaka, kwa kocha aliye
sawa. Nilikuja hapa na nilifurahi sana.."

Mane alipigiwa kura kuwa mchezaji bora wa timu hiyo na
mchezaji bora wa wachezaji katika msimu wake wa kwanza na baadaye akafunga
magoli 10 kati ya yake 20 msimu uliopita katika ligi ya mabingwa wakati
Liverpool ilipofika katika fainali.
Aliichezea timu ya taifa ya Senegal katika mashindano ya
kombe la dunia 2018 nchini Urusi na kufanikiwa kufunga mara moja katika mechi
tatu za nje.
Hivi karibuni ametajwa katika orodha ya wachezaji 30 kwa
tuzo ya Ballon d'Or na ni miongoni mwa wagombea watano wa tuzo ya mchezaji bora
wa soka wa BBC Afrika mwaka huu.
"Siwezi kufikiria klabu yoyote Ulaya ambayo haiwezi
kumtaka mchezaji kama Mane awachezee, kwahivyo kwamba anataka kuendelea kucheza
na sisi, inatoa ujumbe kuhusu sehemu tuliopo kwa sasa," amesema meneja wa
Liverpool, Klopp.
Mkataba wa Mane unafuata mikataba mingine kama hiyo ya muda
mrefu kwa wachezaji wenzake Mane wa kiungo cha mbele, Roberto Firmino,
aliyekubali mkataba huo mnamo Aprili, na Mo Salah, aliyesaini mkataba mpya
Julai.
0 Comments