Serikali
imeifunga Shule ya Sekondari ya Lyamungo iliyoko Hai mkoani Kilimanjaro, baada
ya wanafunzi wake kuzusha vurugu kubwa huku wakivamia na kuivunja ofisi ya
Makamu Mkuu wa shule hiyo.
Kaimu Mkuu
wa Wilaya ya Hai, Onesmo Buswelu, alithibitisha jana kuifunga sekondari hiyo ya
kitaifa kuanzia Machi Mosi hadi Machi 17, mwaka huu.
Shule hiyo
ya kitaifa hupokea wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita kutoka mikoa
mbalimbali nchini.
"Ni
kweli nimeifunga hiyo shule kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na sababu za
kiusalama. kulikuwa na uchaguzi wa serikali ya wanafunzi na wakati unafanyika
mwanafunzi mmoja aliandika matusi makubwa akiwatukana walimu.
"Baada
ya kufanyika uchunguzi aligundulika huyo mwanafunzi na hapo ndiko walipoandaa
vurugu hizo na kujielekeza kuharibu mali na kusababisha hasara ambayo bado
haijafahamika," alisema Buswelu.
Kwa mujibu
wa Buswelu, vurugu hizo ziliibuka baada ya mwanafunzi huyo (jina limehifadhiwa)
kupewa barua ya kufukuzwa shule kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Buswelu ambaye
pia ni Mkuu wa Wilaya ya Siha ameagiza Bodi ya shule hiyo kukutana kesho (leo)
kufanya tathmini ya hali ya uharibifu na madhara yaliyojitokeza na kuiarifu
serikali.
Mpaka sasa,
hakuna mwanafunzi anayeshikiliwa kwa kufanya vurugu na kusababisha hasara ya
mali na rasilimali za serikali.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
Hamisi Issah, alisema wanafunzi hao walifanya tukio hilo saa 4:30 asiku juzi.
"Hao
wanafunzi wameharibu ofisi ya mwalimu huyo ambaye pia ni mwalimu wa nidhamu kwa
kuvunja paa la juu, milango, madirisha na samani za ndani," alisema
Kamanda Issah.
0 Comments