
RAIS John
Magufuli amesema Serikali imebaini kuwa kampuni ya Mawasiliano ya Bharti Airtel
ni mali ya Shirika la Mawasiliani Tanzania (TTCL) na amemwagiza Waziri wa fedha
na mipango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na
serikali.
Rais
ameyasema hayo leo Desemba 20 wakati akizungumza kwenye Ofisi za Taifa za
Takwimu mjini Dodoma.“Kampuni ya AIRTEL imethibitika kuwa ni mali ya Shirika la
TTCL, lakini kuna mchezo ulifanyika, sasa sitaki kuongea sana. Nataka Waziri wa
Fedha ufuatilie suala hili kabla ya mwaka huu kuisha,” amesema Magufuli.
Taarifa na
ndani zinabainisha kwamba hisa za Airtel zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Shirika
la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kuendesha biashara za kampuni hiyo yenye
wateja wengi zaidi nchini ikiwa nyuma ya Vodacom na Tigo.
Chanzo cha
mpango huo kinatajwa kuwa ni uongozi wa juu wa TTCL uliotaka Serikali kudai
haki zake za uwekezaji ndani ya Airtel ambako inaimiliki kwa ubia wa asilimia
40 kwa 60 na mwekezaji.
Taarifa
zinaarifu kuwa TTCL itamiliki hisa zote za Airtel Tanzania Limited ambapo
tayari TTCL imewasilisha hoja ya kutaka kufanya hivyo baada ya kubaini kwamba
Serikali ilipunjwa kwenye hesabu za uwekezaji.
Hoja ya TTCL
inaanzia Novemba 3, 1998 ilipoanzisha kampuni tanzu ya Cellnet ambayo ilifanya
kazi mpaka Mei 7, 2001 ilipobadilishwa jina na kuitwa Celtel Tanzania huku
umiliki wake ukiendelea kuwa chini ya shirika hilo kwa asilimia zote baada ya
kuwekeza Dola milioni tano za Marekani (zaidi ya Sh11 bilioni sasa).
Lakini,
Januari 31, 2002, Celtel ikiwa chini ya umiliki wa TTCL ilikopa kiasi cha Dola
82 milioni (zaidi ya Sh180.4 bilioni) ili kukuza mtaji wake.
Kwa kipindi
hicho, TTCL iliyokuwa na thamani ya Dola 600 milioni (zaidi ya Sh1.32 trilioni)
ilikuwa inamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Kampuni ya Mobile System
International (MSI) ya Uholanzi. Serikali ilikuwa inamiliki asilimia 65 ya hisa
zote na mbia huyo asilimia 35 zilizosalia.
Agosti 5,
2005, mabadiliko yalifanywa kwenye bodi ya wakurugenzi wa Celtel kwa lengo la
kuunda kampuni mbili tofauti; Celtel ikitenganishwa na TTCL. Kutokana na
mabadiliko hayo, Celtel iliwekwa chini ya umiliki wa MSI ambayo Septemba 2007
iliuza hisa zake kwa Zain ambayo nayo ilikuja kuziuza kwa Bharti Airtel, Juni
8, 2010.
Imeelezwa
kuwa TTCL inadai uwekezaji wake ilioufanya Celtel baadaye Airtel ambayo thamani
yake imeongezeka maradufu sasa haulingani na inachokipata hivyo kutaka
kusimamia biashara za kampuni hiyo ya mawasiliano.
Hoja ya
madai hayo ni namna umiliki wa hisa ulivyobadilishwa baada ya Celtel
kutenganishwa na TTCL ambayo ilipewa hisa chache tofauti na ilivyostahili.
Kwa sasa,
Airtel Tanzania inamilikiwa na Serikali yenye asilimia 40 na Celtel Tanzania
BV, kampuni tanzu ya Zain Africa BV ambayo ilinunuliwa na Bharti Airtel
International, Novemba, 2010 ikiwa na asilimia 60.
Katika
mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni, Serikali iliilipa Bharti Airtel Sh14.7
bilioni hivyo kuchukua asilimia 35 ya hisa ilizokuwa inamiliki na kuifanya
imiliki asilimia zote za TTCL.
Sheria mpya
iliyopitishwa hivi karibuni na Bunge imeibadili TTCL inayohudumia asilimia 0.82
ya soko kuwa shirika la umma la mawasiliano na kulipa jukumu kubwa katika sekta
ya mawasiliano nchini.
Bharti
Airtel inatakiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar
es Salaam (DSE) ili kukidhi vigezo vya sheria ya posta na mawasiliano ya mwaka
2010, lakini bado haijafanya hivyo.

0 Comments