Jeshi la
Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija
katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa
likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana
na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua
kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Aidha Jeshi
la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu
pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi
kuhakikisha mkoa wetu unakua mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na matukio kama
ifuatavyo:-
KUKAMATWA
KWA WATUHUMIWA WATATU WAKIWA NA NYARA ZA SERIKALI.
Mnamo tarehe
05 Februari, 2018 majira ya saa 19:45 usiku huko maeneo ya Mwanjelwa, Kata ya
Ruanda, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya likiwa
katika majukumu yake ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, limefanikiwa
kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na nyara za Serikali ambazo ni vipande
vinne vya meno ya Tembo.
Watuhumiwa
waliokamatwa wamefahamika kwa majina ya 1. KENEDY LUPEMBE SIMSOKWE [43]
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT – Tawi la Mbeya na Mkazi wa Iyela 2. MATHEW
ELIKANA MWANJALA [42] Mpiga picha na Mkazi wa Iyela na 3. SHABAN MKWICHE [24]
Mkazi wa Iyunga.
Aidha baada
ya kukamatwa na kupekuliwa, watuhumiwa walikutwa na nyara hizo [Vipande vinne
vya Meno ya Tembo] ambavyo vina uzito wa kilogram 5 na thamani ya Tshs
33,000,000/=.
Taratibu za
kisheria zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi.
WITO:
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito
kwa jamii kuacha tabia ya kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka kwa
kutumia njia za mkato zisizo halali, badala yake wafanye kazi halali ili kupata
kipato halali. Aidha Kamanda MPINGA anatoa rai kwa yeyote mwenye taarifa juu ya
mtu/ watu au kikundi /mtandao wa watu wengine wanaojihusisha na matukio ya
ujangili wazitoe katika mamlaka husika ili hatua za kisheria dhidi yao
zichukuliwe mara moja.
Imesainiwa
na:
[MOHAMMED R.
MPINGA – DCP]
KAMANDA WA
POLISI MKOA WA MBEYA.
0 Comments