Zikiwa
zimepita siku tatu tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam
iwahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela wahamiaji haramu 77 kutoka Ethiopia,
wengine 83 wamedakwa mkoani Iringa huku dereva aliyekuwa akiwasafirisha
akifanikiwa kutoroka.
Wahamiaji
hao walikamatwa wilayani Kilolo mkoani hapa wakiwa safarini kupelekwa Malawi
kisha Afrika Kusini.
Hata hivyo
katika harakati za kukamatwa kwao, dereva wa lori mali ya mkazi wa Tukuyu
mkoani Mbeya alitoroka.
Raia hao wa
Ethiopia walikamatiwa katika Kijiji cha Mbigili ambapo Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, Hope Kawawa alisema walikamatwa juzi saa
kumi na moja jioni karibu na bomba la mafuta la Tazama.
Alisema
wahamiaji hao walipelekwa kituo cha polisi cha Lugalo na kwamba, kukamatwa kwao
kunatokana na taarifa iliyofikishwa Uhamiaji na wananchi.
Alisema
maofisa wa Uhamiaji kwa kushirikiana na polisi walipowakamata baadhi yao
waliwakuta hali zao ni mbaya kutokana na kukosa chakula kwa siku tatu na pia
kuathiriwa na joto kutokana na bodi la lori walilokuwa wakisafiria kuwa la
bati.
“Wahamiaji
hawa walikuwa wanasafiri kwenye lori mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya,
dereva alikimbia na hajapatikana lakini uchunguzi unaendelea,” alisema.
Aliongeza
kuwa wahamiaji hao watafikishwa mahakamani kesho kujibu mashtaka
yanayowakabili.
“Naomba
niwaambie madalali wanaosafirisha hawa wahamiaji kuwa mkoa wa Iringa si mahala
salama kuwapitisha kwa kuwa tuko makini saa 24 na tukiwabaini hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Alitoa wito
kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapohisi baadhi ya watu si raia wa Tanzania
na wanapowaona watu wasiowatambua. Mtanzania aliyekamatwa akihusishwa na
usafirishaji wa wahamiaji hao, Hassan Mwalusanjo alisema hana anachofahamu.
Alisema
aliomba lifti katika gari hilo kutoka Tukuyu kwenda Dar es Salaam kununua vifaa
vya gari wakati gari hilo lilipokuwa likisafirisha ndizi. Mwalusajo alisema
baada ya kushusha ndizi eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, dereva aliondoka
na aliporeja alipanda kurejea Tukuyu.
Alisema
walipofika Ilula alishuka kula ndipo dereva alipoondoka na gari na aliporejea
alimuomba amsaidie kusafisha gari.
“Sielewi
chochote nilishangaa kuwekwa chini ya ulinzi baada ya dereva kuniambia
nimsaidie kusafisha gari ambako nilikuta makopo ya maji na mifuko ya mikate,”
alisema akiwa chini ya ulinzi.’’
0 Comments