Jeshi la
Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, linawashikilia waganga wa jadi wawili
ambapo mmoja ni mkazi wa Kijiji cha Obwere na Michael Jacob wa Omuga kwa tuhuma
za kumjeruhi kwa kumuunguza moto, Emiliana Thomas anayeishi Kijiji cha Omuga
wilayani Rorya.
Kamanda wa
Polisi wa mkoa huo, Henry Mwaibambe alisema jana kuwa, majeruhi huyo ambaye ni
mwanamke anayesumbuliwa na tatizo la kutopata ujauzito, waganga hao walimwaminisha
kuwa ataupata.
Alisema
walimwambia ili apate mtoto ni mpaka kuku imwagiwe mafuta ya taa na iteketezwe
moto huku mama huyo akiwa ameishikilia mikononi.
Kamanda
alisema baada ya waganga hao kuwasha moto ulimunguza na kumsababishia majeraha.
Mwaibambe
alisema, awali waganga hao walimweleza mwanamke huyo kuwa anasumbuliwa na
mashetani ndani ya tumbo na ndio yanayomfanya asizae.
Alisema
walimweleza kwamba kuku ikiteketea ikiwa mikononi mwake atakuwa ameondokana na
mashetani, hivyo ni lazima iteketezwe.
Kamanda huyo
alisema baada ya waganga hao ‘kumsomesha’ mwanamke huyo alikubali na ndipo
walipoimwagia mafuta ya taa kuku hiyo na kuwasha moto kwa kibiriti uliolipuka
na kumjeruhi kifuani na mikononi.
Mwaibambe
aliongeza kuwa, hali ya mama huyo ni mbaya na anaendelea na matibabu katika
Hospital ya Kowak wilayani humo.
Mmoja wa
waganga hao wa jadi, Jacob alisema tukio hilo ni ‘bahati mbaya’.
“Alikuja
akiomba tiba, sasa kwa bahati mbaya mafuta yalikuwa yamemumwagikia mikononi na
mikono ya nguo aliyokuwa amevaa ilikuwa hadi mikononi, wakati tumewasha moto
ndipo ukamuunguza,” alisema Jacob.
Mwakilishi
wa Chama cha Tiba Asili mkoani Mara, Jacob Matiko alilaani kitendo hicho kuwa
hakiendani na taratibu za tiba na kinakiuka sheria inayozuia vitendo hivyo huku
akiwataka waganga kutofanya utapeli iwapo hawawezi kufanya tiba kama matabibu
asili.
0 Comments