Baada ya
mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Katibu wa Chadema Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano
jela, wakili wao Peter Kibatala amesema wanakusudia kukata rufaa.
Sugu na
Masonga wamehukumiwa adhabu hiyo leo Februari 26,2018 na Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite.
Wawili hao
wamehukumiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli,
kosa walilotenda kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la
Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.
Kibatala
amesema baadaye watatoa taarifa ya nini kinaendelea ila wanakusudia kukata
rufaa.
Baada ya
hukumu kutolewa viongozi wa Chadema waliokuwepo mahakamani waliingia kwenye
magari yao na kuelekea katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini.
Wakati wa
usomwaji wa hukumu hiyo, nje ya jengo la mahakama ulinzi uliimarishwa kukiwa na
askari waliotanda hadi maeneo ya jirani.
Sugu ni
mbunge aliyeweka rekodi ya kupata kura nyingi kuwashinda wabunge wote wa
majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika
uchaguzi huo, Sugu alipata kura 108,566 akiwaacha wapinzani wake kugawana kura
57,690.
Hukumu
imetolewa na hakimu Mteite aliyesikiliza shauri hilo baada ya upande wa
mashtaka na wa utetezi kukamilisha ushahidi Februari 9,2018.
Jamhuri
iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa
kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.
Upande wa
utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka
maneno waliyoshtakiwa kuyatoa.
Washtakiwa
walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla
ya kujitoa na kazi hiyo kufanywa na Kibatala.
Kwa mara ya
kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa
mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph
Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na
usikilizaji.
0 Comments