Mahakama ya
hakimu mkazi Mkoa wa Dodoma imemwachia mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Vijana
wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis baada ya upande wa Jamhuri
kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi iliyokuwa ikimkabili.Uamuzi huo umetolewa
leo Februari 15, 2018 na hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Emmanuel Fovo baada
kuridhia ombi la wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Biswalo Biswalo kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo.Desemba 9, 2017, Sadifa
alikamatwa na Takukuru akiwa nyumbani kwake Mailimbili mjini hapa akituhumiwa
kugawa rushwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo.Mbunge huyo wa Donge na
mjumbe wa kamati kuu ya CCM aliyemaliza muda wake, baada ya kukamatwa alilala
mahabusu kwa siku tatu baada ya kukosa dhamana.Katika shtaka la kwanza, Sadifa
alidaiwa aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed Rashid ambaye
alikuwa akiwania umakamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja huo.Shtaka la
pili, alidaiwa kuwaahidi kuwalipia gharama za usafiri wanachama wa umoja huo
kwa kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid.
0 Comments