Ndugu wa
mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline
aliyepigwa risasi na Polisi Februari 16, 2018 wameeleza ndugu yao alifariki
dunia baada ya kupigwa risasi kichwani.
Wametoa
ufafanuzi huo leo Februari 19, 2018 muda mfupi baada ya kususa kupokea mwili wa
mwanafunzi huyo uliokuwa ukifanyiwa uchunguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH) bila kuelezwa nini kilichomuua.
Wakizungumza
mara baada ya maafikiano baina yao na madaktari, wamesema wamepewa sehemu ya
ripoti ya uchunguzi ambayo wameridhika nayo na sasa wanakwenda kufanya kikao
cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.
Shemeji wa
mwanafunzi huyo, Festo Kavishe amesema uchunguzi wa mwili huo, umeonyesha
kwamba Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.
"Ripoti
ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa vibaya na
risasi ambayo iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande
wa kulia ambao umefumuka vibaya," amesema.
Kwa mujibu
wa Kavishe, iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo wasingethubutu kuuchukua
mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji kupata picha kamili ya nini
kilimuua Akwilina.
"Sasa
tumeshafahamu nini hasa kimemuua ndugu yetu kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na
madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi
yake," amesema Kavishe.
Akwilina
alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye
daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.
0 Comments