Kiongozi wa
kikundi cha wapiganaji wa Boko Haram Abubakar Shekau, ameonekana kwenye video
mpya karibu saa ishirini na nne baada ya Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kwa
mara ingine kutamka hadharani kuwa kikundi hicho kimesambaratishwa.
Huu ni
mkanda wa video wa kwanza kutolewa na Shekau baada ya kimya cha miezi kadhaa
iliyopita, naye ni mongoni mwa viongozi wanaosakwa kwa hamu na ghamu na kupewa
sifa ya kuwa miongoni mwa magaidi wanaosakwa na Marekani pamoja na mamlaka ya
Nigeria.
Abubakar
Shekau anaonekana kwenye mkanda huo wa video akiwa ameketi peke yake akiwa
amevalia kanzu,kofia yenye rangi inayofanana na bunduki aina ya AK-47 ambayo
anaonekana kuwa na mahaba nayo.Lakini anaonekana kushindwa kuzungumza kwa sauti
yenye mamlaka ikilinganishwa na matamko yake ya awali .
Akisoma
kutoka katika karatasi kwa lugha ya kiarabu na ki Hausa, Shekau, anakiri kundi
lake kuhusika katika matukio ya hivi karibuni nchini Nigeria katika maeneo ya
kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo ikiwemo lile lililotukia siku ya siku kuu ya
Christimas katika kijiji cha Molai nje ya jiji la Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo
la Borno.
Shekau
alijinasibu kwa kusema kuwa askari wa kundi la wanamgambo la Boko Haram wana
afya maridhawa na kwamba vikosi vya ulinzi nchini Nigeria haviwezi kufanya
lolote dhidi ya wanamgambo wake.
Sehemu ya
dakika thelathini na moja ya mkanda huo zimeoneshwa mbwembwe za wapiganaji wa
kundi hilo ikiwemo magari ya silaha, malori na pikipiki huku wakinapiga risasi
hewani kwa kile kinachoonekana kizuizi cha njiani katika kambi ya kijeshi
iliyotelekezwa .
Wakati huo
huo Shekau alionekana akitoa tamko juu ya kukerwa kwake dhahiri juu ya
kutambuliwa hivi karibuni mji wa Yerusalemu kama mji mkuu wa Israeli tamko
lililotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump, Abubakar Shekau, ameijosoa nchi
ya Saudi Arabia kwa kushirikiana na wale aliowaita makafiri na kuwalaumu
Wapalestini kwa uharibifu wao.
Mpaka sasa
serikali ya Nigeria haijatoa tamko lolote juu ya mkanda huo wa video na ujumbe
uliomo ndani yake. Hata hivyo jeshi la Nigeria linakiri kuwafukuza waasi kutoka
katika ngome zao kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, hata hivyo wanamgambo wa
kikundi cha wapinaji cha Boko Haram bado wanaendeleza mashambulizi ya kujitoa
muhanga , mashambulizi ya risasi za moto zaidi wakilenga vifaa vya kijeshi na
vijiji.
0 Comments