
Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi
kwa matibabu mwezi mmoja kuanzia sasa.
Familia yake
imesema Lissu baada ya kupata matibabu nje ya nchi amepanga kufanya mambo
matano akirejea salama .
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23, kaka wa Tundu Lissu, Wakili
Alute Mughwai alisema taratibu za kumsafirisha nje ya nchi zimeanza.
Lissu,
ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu na mwanasheria mkuu wa chadema amelazwa katika
Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30
alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba7.
"Awamu
ya tatu ya matibabu yake ni maalumu sana kwani itahusu pia mazoezi ambayo kama
haitafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa kudumu,"alisema.
Hata hivyo,
alisema Lissu atapelekwa nje kwa ndege ya kawaida tofauti na hali yake ya awali
alipotakiwa kusafirishwa na ndege maalumu za wagonjwa.
"Itatolewa
taarifa ni lini ataondoka kwa matibabu na atakwenda nchi gani, hasa baada ya
kupata ushauri wa mwisho wa madaktari katika hospitali Nairobi," alisema.
Mughwai
alisema amezungumza na Lissu akiwa Hospitali Nairobi na amemueleza kuwa
akirejea tu nchini, kuna mambo makubwa matano ambayo atafanya.
Alisema
jambo la kwanza, ambalo atafanya ni kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
kuwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kuokoa maisha yake siku
aliyopigwa risasi.
Wakili
Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na msikitini
kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada maalumu.
"Baada
ya ibada, tutaangalia utaratibu kifamilia kama itawezekana kwenda kufanya
matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika vita miaka 200
iliyopita," alisema.
Alisema
baada ya hapo, anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale
alipoishia kwa ari kubwa .
Wakili
Mughwai alisema jambo la tano atahakikisha anasimama na kupambana kisheria na
watu waliotaka kukatisha maisha yake baada ya kumpiga risasi.
"Amesema
atahakikisha anasimamia jambo hili kwa uwezo wake wote ili kuhakikisha
wanafikishwa katika vyombo vya sheria waliohusika na uovu huo," alisema.
Familia
yataka Lissu akahojiwe Nairobi
Akizungumzia
juu ya upelelezi wa shauri la Lissu, Mughwai alisema bado msimamo wao upo
palepale wanaomba wapelelezi kutoka nje ya nchi washirikiane na wapelelezi wa
ndani kuwakamata watuhumiwa.
Alisema
ingawa familia ya Lissu iliandika barua tangu Septemba 16, kutaka wapelelezi wa
kimataifa na kujibiwa na mwanasheria mkuu Septemba 20 kuwa jukumu la upelelezi
ni la polisi.
"Tunataka
wapelelezi wa nje kushirikiana na wa ndani kwa sababu hatuna imani na upelelezi
kutokana na kasi ndogo kwani hadi sasa wamekuwa wakieleza kukwama upelelezi
kutokana na kutomuhoji dereva wa Lissu,"alisema.
Hata hivyo,
alisema kwa sasa Lissu anaweza kuongea mwenyewe hivyo, jeshi la polisi linaweza
kwenda Nairobi kumuhoji na atawapa maelezo yote ikiwepo watu ambao aliwatambua.
"Bila
shaka Lissu atawaeleza watu hao, walimshambulia kwa sababu gani,"alisema.
Familia
yaelezea gharama
Katika hatua
nyingine, Mughwai alisema Oktoba 2, familia ya Lissu ilikutana na viongozi wa
bunge kujadili matibabu yake ambayo ni haki yake kisheria.
Alisema
baada ya mazungumzo hayo, Oktoba 8, familia iliandika barua rasmi kwa katibu wa
bunge kwa kuzingatia sheria ya bunge namba 14 kifungu cha 24 kuhusu stahiki za
mbunge.
Alisema
barua hiyo, ilipelekwa bungeni kwa kutumia shirika la kubeba mizigo na vifurushi
la DHL na kupokelewa Oktoba 19 na baadaye aliwasiliana na Spika Job Ndugai na
kumweleza juu ya barua hiyo na aliahidiwa kuwa suala hilo litashughuliwa.
Hata hivyo,
alisema familia haijapata mrejesho tangu wakati huo hadi Novomba 11, alipoamua
kumpigia katibu mpya wa bunge baada ya kushauriwa na Spika Ndugai ambaye
aliahidi kufuatilia.
"Hivyo
hadi sasa bado Bunge halijaanza kugharamia matibabu ya Lissu kama sheria
inavyosema na Lissu amekuwa akitibiwa kwa michango ya watu mbali mbali,"
alisema
Alisema
michango hiyo ambayo inakusanywa katika akaunti maalumu ya Chadema na pia
kupitia chama cha mawakili(TLS) ndio hadi sasa inatumika.
"Tutaendelea
kulitaka Bunge kugharamia matibabu kwani sio suala la hiari, ni haki ya mbunge
lakini pia tunaomba wananchi waendelee kuchangia matibabu ya Lissu kupitia
akaunti iliyotolewa na Chadema, chama cha TLS na kwa familia"alisema
Akanusha
mgawanyiko juu ya matibabu
Katika hatua
nyingine, Mughwai alisema, familia ya Lissu, Chadema na chama cha Mawakili wa
Tanganyika(TLS), hawana mgawanyiko wowote juu ya matibabu ama hatua
zinazoendelea za kumtibu Lissu.
Wakili
Mughwai alisema wanasikitishwa na taarifa kuwa familia imegawanyika juu ya
uamuzi wa kuliomba bunge kugharamia matibabu ya Lissu.
"Tupo
kitu kimoja wote familia yetu tupo pamoja kwa yote na Lissu anajua hatua zote
kwani hata makamishna wa bunge walipomtembelea Oktoba 23 aliwauliza kuhusu
stahiki zake kama mbunge,"alisema.
Tundu Lissu
alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nje ya nyumba yake akirejea kutoka
vikao vya bunge Dodoma, Septemba 7 na kukimbizwa hospitali ya Nairobi kwa
matibabu ambapo hadi sasa anapatiwa matibabu.

0 Comments