TUPO kwenye Ligi Kuu Bara, kipindi ambacho kilikuwa
kinasubiriwa kwa hamu kubwa ikiwa ni msimu wa 2023/24.
Mashabiki wa mpira nchini walisubiri kwa hamu kubwa kuona
ligi inaanza tena. Hilo likatokea na tumefanikiwa kuona mambo yakienda vizuri
sana.
Ligi imekuwa na msisimko mkubwa licha ya kwamba, mabingwa
watetezi Yanga wameshindwa kuanza mechi za ligi baada ya kupewa nafasi ya
kujiandaa katika michuano ya kimataifa.
Mechi yao ya jana ikiwa ni hatua ya awali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika, Yanga ndio walikuwa wanaanza kazi dhidi ya Telecomunication ya
Djibouti.
Wawakilishi wengi wa Tanzania katika michuano hiyo, Simba
wao wataanzia hatua inayofuata, hii ni kutokana na pointi walizozikusanya na
zinawafanya wawe na nafasi hiyo pamoja na timu nyingine kubwa za Afrika.
Wakati Yanga hawajaanza ligi katika mechi ya pili sasa,
wengine wameanza na unaona. Kama kutakuwa na mapungufu basi yatakuwa machache
ya kibinadamu.
Hapa sigusi yale mapungufu ya uzembe yaliyofanywa na uongozi
wa klabu ya Kitayose kushindwa kukamilisha usajili wa wachezaji wake.
Nazungumzia mengi, kwa maana ya viwanjani na kadhalika.
Lakini zaidi leo kwa mara nyingine bila kuchoka nagusia suala la waamuzi.
Hakuna matukio ya kukera kwa uzembe, matukio ambayo kama
unayakumbuka yalikuwa rundo katika mzunguko wa kwanza wa msimu uliopita.
Malalamiko ya timu nyingi sana yalikuwa makubwa. Waamuzi
walifanya makosa makubwa mengi yaliyopitiliza.
Hakika yalikuwa makosa yanayojirudia kwa baadhi ya timu
dhidi ya timu ambazo zilipolalamika hakukuwa na ubishi ulikuwa ukweli mtupu.
Faida ya mikwaju ya penalti ambayo wazi ilionekana ilikuwa
kuna walakini mkubwa na wa wazi. Kuna timu zilifaidika na kukawa na marudio ya
timu hizo kufaidika na kupatikana kwa mikwaju hiyo lakini ya uonevu.
Kuna viwanja vilikuwa maarufu, wanapocheza wenyeji, waamuzi
“walinyonga” hadharani bila ya woga. Jambo ambalo halikuwa sahihi hata kidogo
na bado wakaendelea kufanya hivyo.
Hakuna tunachoweza kukataa kwamba rushwa ipo, tunajua tayari
Takukuru wamesema wameingia na watashirikiana na TFF katika hili lakini lazima
tuwe wakweli, kazi ni ngumu kwa kuwa wanaotoa na wanaopokea “wote wanafurahia”.
Hivyo inakuwa kazi ngumu kwao kuzuia hili au kuwapata hawa
watu ambao wamekuwa na tabia hizi mbovu na si za kuiungwana ambazo zinaharibu
mpira wetu.
Nimeona leo itakuwa ni nafasi nzuri ya kuwakumbusha, kwamba
baadhi ya waamuzi waliposimamishwa, mambo yakatulia na tukaenda kwa mwendo
mzuri sana.
Haikuelezwa lakini ukweli wako walikuwa kama mawakala wa
baadhi ya klabu ambazo zilifaidika sana na “wizi wa hadharani”.
Inawezekana wamerejea na inawezekana wakawa wameahidi kwamba
wamejirekebisha kwa nia ya kuhakikisha wanafanya vema baada ya kuweka sawa
mienendo yao mibovu.
Sijajua kama TFF na Kamati ya Waamuzi watakuwa
wamewarudisha. Na kama itakuwa ni hivyo basi tuwaonye mapema kwa kuwa bado tuna
kumbukumbu mbovu dhidi yao.
Tunawakumbusha waache kufanya makosa ya makusudi na kuyaita
makosa ya kibinadamu. Tunawakumbusha kuacha kuuharibu mpira wa Tanzania kwa
makusudi kwa maslahi yao binafasi.
Mwisho, mimi niwakumbushe kuisimamia haki kwa dhati kama
ambavyo walivyoaminiwa kuwa watafsiri wa sheria 17 za mchezo wa soka uwanjani.
Jukumu ni kubwa na haki inatakiwa kupita kiasi. TFF
hawatachafuka kama waamuzi watakuwa bora na wakumbuke, ligi yetu sasa ni
maarufu zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Hivyo haipendezi kuwa
na gumzo la maamuzi mabovu kutoka kwa waamuzi walioaminiwa na kamati ya waamuzi
na wakapewa kazi chini ya shirikisho la soka.
Ninaamini kuna nafasi kubwa mambo yakawa sahihi na bora kama
waamuzi wataifanya kazi yao kwa weledi. Niwakumbushe, mpira unachezwa hadharani
na makosa yote yanaonekana wazi kuwa ni ya kibinadamu au makusudi kwa maslahi
binafsi.
Source: Saleh Ally Jembe
0 Comments