Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Mbunge wa Nanyamba
(CCM), Abdallah Chikota, ameomba kuunda Tume huru ya kuchunguza kushuka kwa
uzalishaji wa zao la korosho ndani ya miaka mitatu mfululizo licha ya jitihada
za kupanua wigo wa kilimo cha zao hilo kwenye mikoa mbalimbali.
Akichangia jana mjadala
wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa
mwaka 2023/24, Mbunge Chikota alisema pamoja na jitihada za serikali za
kuratibu upatikanaji wa pembejeo kuna mdondoko wa zao hilo.
“Napongeza serikali ya
awamu ya sita kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuwekeza katika tasnia ya
korosho, tumeona kwa miaka mitatu mfululizo, Serikali ikitoa pembejeo bure kwa
wakulima wa korosho, tunaendelea kuishukuru Serikali.”
“Mwaka huu kuna
mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 340 ambayo imetolewa na nina matumaini
pembejeo hizi zitafika kwa wakati na wakulima wa korosho watanufaika na
pembejeo,”alisema Chikota.
Kadhalika, alisema
pamoja na uwekezaji ulifanywa na serikali kwenye tasnia ya korosho bado kuna
anguko la uzalishaji wa korosho nchini ambapo kwa kwa msimu wa kilimo wa mwaka
2017/18, Tanzania ilifikisha uzalishaji wa tani 320,000.
“Lakini kwa masikitiko
makubwa katika msimu uliopita uzalishaji umepungua hadi kufikia tani 160,000
pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa, ukiuliza Bodi ya Korosho hawana majibu
ya uhakika na hata taasisi ya utafiti ya TARI Naliendele hawana majibu ya
kutoshereza ya anguko kubwa na uzalishaji wa korosho,”alisema.
Alisisiza “Haiwezekani
mikoa ya uzalishaji wa korosho imeongezeka, serikali imefanya uwekezaji wa
kutosha lakini uzalishaji unazidi kuwa mdogo.”
Chikota alisema malengo
ya Bodi ya Korosho mwaka huu ilikuwa ni kufikisha tani laki nne na Ilani ya
Chama cha Mapinduzi na kufikisha tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
“Kwa anguko hili kuna
kazi kubwa inayopaswa kufanywa ili kufikia malengo nashauri serikali kuunda
tume hii huru yenye wataalamu kutoka nje ili kupata mawazo mapya,”alisema.
Aliomba watumie
wataalamu wa nje na SUA ili kuangalia mfumo wa uagiziaji na udhibiti wa
pembejeo kwa kuangalia ubora wake.
“Tusiendelee kuwatumia
wataalamu wale wale wa TARI na Bodi ya Korosho watatuletea majibu yela yale
tuliyoyazoea. Tupate timu mpya, ikiwezekana tuchukue uzoefu kutoka
huko,”alisema.
Pamoja na hayo, Chikota
aliishauri Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara na reli ili kufungua
mikoa ya kusini.
Pia alishauri Serikali
kutekeleza mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma ili kuweza upatikanaji wa maji hatua
ambayo itavutia wawekezaji.
0 Comments