MAMLAKA za
Kenya, jana zilizima vituo vya televisheni kuzuia matangazo 'live' ya sherehe
za kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ambaye alisusia uchaguzi
wa marudio wa mwaka jana uliobishaniwa.
Alijitangaza
kuwa "rais wa watu" mbele ya maelfu ya wafuasi wake katika mji mkuu
wa Nairobi.
Matokeo ya
uchaguzi mkuu wa Agosti, mwaka jana, yalibatilishwa kutokana na madai ya
ukiukwaji wa kanuni.
Uhuru
Kenyatta alishinda uchaguzi wa marudio Oktoba, lakini Odinga hakushiriki, hivyo
Kenyatta aliapishwa kuongoza muhula wa pili Novemba, mwaka jana.
Alivionya
vyombo vya habari kutotangaza shughuli ya jana na mwanasheria wa serikali
alisema kufanya hafla hiyo ni kosa la uhaini.
Hata hivyo,
vituo vikuu vya TV vilionyesha tukio hilo kupitia mitandao yake ya kompyuta,
kwenye YouTube na Facebook.
Akiwa
ameshika Biblia mkono wake wa kulia katika bustani ya jijini Nairobi, Odinga alitangaza
kuwa anajibu "wito wa ngazi ya juu kuchukua ofisi ya rais wa watu wa
Jamhuri ya Kenya."
Watu
wamechoshwa na wizi wa kura katika uchaguzi na tukio hilo lilikuwa hatua
kuelekea ujenzi wa demokrasia sahihi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki,
Odinga aliuambia umati uliokuwa ukishangilia.
Aliyekuwa
mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, hakuwapo kwenye hafla hiyo. Odinga
alisema ataapishwa siku nyingine.
Akizungumza
awali na televisheni ya Kenya ya KTN, Odinga alisema kufungwa kwa vyombo vya
habari "kumethibitisha kuwa tumeporomoka kufikia kiwango cha Uganda",
ambayo ilisimamisha matangazo ya vyombo vya habari wakati wa uchaguzi mwaka
2016.
"Kuapishwa
kwake" kulikuwa na lengo la "kuonyesha dunia kuwa tunachofanya ni
halali kisheria, kikatiba na kitu ambacho huwezi kukielezea hata kidogo kuwa
mapinduzi", alisema zaidi.
Vituo vitatu
binafsi vya televisheni - NTV, KTN na Citizen TV - vilizima matangazo kuanzia
saa 3:10 asubuhi.
Citizen TV
iliiambia BBC kuwa mamlaka za serikali ziliwalazimisha kuzima matangazo
kutokana na mipango ya kuonyesha mkusanyiko huo.
Watazamaji
wa KTN walishuhudia vioo vya luninga zao vikishika rangi nyeusi wakati
mtangazaji akisoma taarifa kutihibitisha kuwa mamlaka ya mawasiliano ilikuwa
ikizima matangazo.
Kuzimwa kwa
'signo' ya matangazo ya vyombo vya habari si jambo la kawaida hapa Kenya.
Palikuwa na
wasiwasi jana huku baadhi ya shule katika mji mkuu wa Kenya zikifungwa kwa
sababu ya tukio hilo, na watu kutojua nini kingetokea.
Polisi awali
walizingira viwanja hivyo, lakini baadaye wakaondoka.
Chanzo: BBC
0 Comments