Wakuu wa
nchi na Serikali za Afrika, wakiwemo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),
mapema mwakani wanatarajiwa kusaini makubaliano ya kuanzishwa kwa eneo huru la
biashara la bara hilo (CFTA).
Wanatarajiwa
kuwa na mkutano wa 30 wa kawaida Januari 28 na 29 mwakani katika ukumbi wa
Nelson Mandela uliopo kwenye Kituo kipya cha Mikutano (AUC) jijini Addis Ababa,
Ethiopia.
Mkutano huo
utakaokuwa nakaulimbiu; “Kushinda Vita Dhidi ya Rushwa: Mwelekeo Endelevu wa
Mabadiliko Afrika,” utatanguliwa na mkutano wa 35 wa Kamati ya Wawakilishi wa
Kudumu (Januari 22-23) na mkutano wa 32 wa kawaida wa Baraza la Utendaji
(Januari 25-26).
CFTA itakuwa
soko la zaidi ya watu bilioni 1.3 na wanatarajiwa kufika takribani bilioni
mbili ifikapo mwaka 2025. Yatakaposainiwa, makubaliano hayo ya kibiashara
yatakuwa makubwa zaidi barani humo yakizihusu nchi zote 54 za Afrika, na
yatakuwa ya pili kwa ukubwa duniani. Makubaliano makubwa zaidi duniani ni ya
Shirika la Biashara la Dunia (WTO) yaliyosainiwa mwaka 1994.
Kwa sasa
Afrika ina masoko mawili makubwa yanayozihusu baadhi ya nchi, ikiwemo Soko la
Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko la Pamoja la Mashariki na
Kusini mwa Afrika (COMESA).
EAC yenye nchi
sita wanachama za Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Tanzania na Kenya, ina
zaidi ya watu milioni 170. Mkutano wa 18 wa kawaida wa wakuu wa nchi na
Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia Januari
2012, uliamua kuwa hadi mwaka 2017 CFTA iwe imeanzishwa. Majadiliano kuhusu
uanzishwaji huo yalianza rasmi Juni 2015.
Juni mwaka
huohuo, wakati wa mkutano wa 25 wa wakuu wa nchi za AU uliofanyika Afrika
Kusini, viongozi hao walikubaliana lianzishwe eneo huru la biashara ifikapo mwaka
2017 kupitia makubaliano na biashara huria za bidhaa na huduma.
Kwenye
mkutano wa nne wa mawaziri wa biashara kutoka nchi za Afrika, uliofanyika hivi
karibuni Niamey, Niger viongozi hao waliidhinisha muundo wa makubaliano na
kuzingatia maendeleo, yaliyofikiwa kwenye majadiliano ikiwa ni sehemu ya
maandalizi ya mkutano ujao wa wakuu wa nchi na serikali. CFTA itatoa uhakika wa
mazingira ya uwekezaji, maendeleo ya viwanda na ongezeko la thamani ya bidhaa
na huduma, hivyo kutengeneza fursa za ajira na vipato vya familia.
Hivi
karibuni, wakati anafungua mkutano wa mawaziri mjini Niamey, Rais wa Jamhuri ya
Niger Issoufou Mahamadou alipongeza maendeleo yaliyofikiwa katika majadiliano
kuhusu makubaliano hayo.
CFTA na
makubaliano mengine yakiwemo ya Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (AIDA),
Programu ya Maendeleo ya Kilimo Afrika (CAADP), Mpango wa Programu ya Maendeleo
ya Miundombinu Afrika (PIDA) vitaiwezesha Afrika kufanikiwa katika malengo ya
mabadiliko.
Makubaliano
ya kuanzisha eneo huru la biashara Afrika, yanaweka ajenda kwa ajili ya
mijadala kuhusu biashara ya bidhaa, biashara ya huduma na utatuzi wa migogoro.
CFTA itashughulikia itifaki mbili, ikiwemo ya biashara ya bidhaa na itifaki ya
biashara ya huduma. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuboresha biashara baina ya
nchi za Afrika.
Malengo
makuu ya CFTA ni kuiwezesha Afrika kuwa na soko moja la bidhaa na huduma,
litakalotoa uhuru kwa wafanyabiashara na uwekezaji na hivyo kutoa fursa ya
kuongeza kasi ya kuanzisha umoja wa forodha barani humu.
0 Comments