Mahakama Kuu
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemhukumu kwenda jela miaka miwili
muigizaji wa filamu bongo Elizabeth Michael (Lulu) ambaye alikuwa anakabiliwa
na kesi ya kuua bila kukusudia.
Hukumu hiyo
imetolewa leo na Jaji Sam Rumanyika aliyekuwa anaendesha kesi hiyo, na kusema
kwamba mshtakiwa amekutwa na hatia ya kuua bila kukusudia kutokana na ushahidi
wa mazingira, hivyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
"Ushahidi
wa mazingira unaweza kutumika kama msingi pekee wa kumtia hatiani mshtakiwa
tena mshtakiwa pekee, sasa ninapokwenda kuangalia maelezo ya mshtakiwa kama
yanakidhi vigezo nilivyosema awali, kwa mujibu wa mshtakiwa alisema alianza
kupigwa na marehemu, marehemu alilewa lakini kuhusu mshtakiwa anatakiwa kutoa
maelezo yanayo jitosheleza, kwa hili mshtakiwa alijikanganya" amesema Jaji
Rumanyika.
Jaji
Rumanyika ameendelea kwa kusema kwamba.."mshtakiwa katika maelezo yake
hakueleza kuwa marehemu alianguka au laah wakati anamkimbiza, maelezo ya Dkt.
Josephine siyo maelezo ya cheti cha hospitali, hayakuwa na hadhi ya
hospitali".
"Inakinzana
na hekima ya kawaida kwamba hata pale marehemu alipoendelea kumpiga na
kumshambulia na akaenda kiwango cha kumtishia kumuua, mstakiwa hakuthubutu hata
kumpiga, ina maana alifanya kama maneno ya biblia yanavyosema mtu akikupiga
shavu la kushoto mgeuzie na la kulia lakini hili mshtakiwa hakulisema.",
amesema Jaji Rumanyika.
"Na
wakati huo mshtakiwa alikuwa na miaka 17, leo ana miaka 22, alikuwa mtoto hivyo
asingetambua kuwa kinachofanyika ni kibaya au kizuri, huyu mtoto sio mshtakiwa
aliyelengwa nasheria ya watoto, kama mtoto wa umri huu na anaweza kafanya ya
watu wazima, mahakama hii haikubaliani bali mshtakiwa ni mkomavu, hakuna
mashaka kuwa kifo cha marehemu kilitokana na ugomvi", ameendelea kusema
Jaji Rumanyika mahakamani hapo.
Baada ya
hapo jaji rumanyika aliwapa nafasi upande wa mshtakiwa kujitetea ambapo wakili
wake Peter Kibatala alimtetea mshakiwa kwa kusema kuwa mshtakiwa anategemewa na
familia yake.
Baada ya
hapo Jaji Rumanyika alitoa hukumu yake na kumuamuru mshtakiwa kwenda jela kwa
miaka miwili.
Elizabeth
Michael (Lulu) anahukumiwa kwa kumuaa aliyekuwa mpenzi wake Steven Charles
Kanumba ambaye pia ni muigizaji mwenzake, mnamo April 7, 2012.


0 Comments